Ndugu
Mhariri ni imani yangu kuwa utanipa nafasi nijibu baadhi ya hoja za
Mayage zenye sura ya upotoshaji kwa manufaa ya wasomaji wako na
Watanzania wenye nia ya kujua ukweli kwa ujumla. Ni imani yangu
utachapisha majibu hayo kikamilifu ili upande wa pili wa shilling
ufahamike kwa wasomaji wako na wananchi kwa ujumla..
Mimi ni msomaji wa Gazeti letu la
Raia Mwema na
magazeti na mitandao mbalimbali hivyo kufuatilia mijadala mbalimbali.
Kila nilipoona dalili ya upotoshaji nimekuwa nikijaribu kuweka
kumbukumbu sawa. Siku za karibuni nimekuwa nikifuatilia makala
zilizokuwa zikitolewa na Mayage S. Mayage kwenye
Raia Mwema.
Makala ya mwisho ilitoka katika
Raia Mwema la Desemba 7 hadi 13, 2011, ukurasa wa 22. Baada ya kusoma makala yake ya kwanza nilimwandikia ujumbe mfupi wa
sms.
Kimsingi nikimshauri asipende kufanya mahitimisho kwenye mambo mazito
na hasa yanayohusu jamii na taifa kwa ujumla bila kufanya utafiti.
Kabla hata toleo la gazeti lililofuata halijatoka nikaanza kupokea simu na
sms kutoka kwa watu waliojiita wapenzi wa CHADEMA, wakilalamikia ujumbe wangu wa
sms kwa Mayage.
Nilistuka sana na kujiuliza maswali yafuatayo; mosi, kama ni kweli waliokuwa wakiniandikia
sms na kunipigia simu ni wapenzi wa CHADEMA walijuaje majibu yangu ya
sms kwa Mayage, kabla gazeti linalofuata halijatoka? Je, walipewa na Mayage na kama ni hivyo, kwa lengo gani?
Pili, lugha iliyotumika kwa wote japo walijitambulisha kuwa sehemu
mbalimbali za Tanzania ilifanana na hakuna hata mmoja aliyejielekeza
kwenye hoja ya msingi kuwa, Mayage ametoa hitimisho bila kufanya
utafiti.
Iweje wote wana lugha inayofanana walikaa wapi kujadiliana na
kupanga ujumbe wa kunitumia? Iweje wote hakuna anayezungumzia hoja
yangu ya msingi, bali msisitizo ni katika walichokiita “kumtukana
Mayage? Hili nalo liliashiria upungufu mkubwa kwa kuwa hitimisho
lisilotokana na utafiti wa kina daima lina upungufu mkubwa, hasa katika
jambo zito kama mikakati ya chama.
Je, watu hao walitarajia mikakati ya chama ingeliwekwa hadharani? Ni
jeshi la ajabu linaloweka mikakati yake hadharani? Ni kwa msingi
huo, nilitarajia Mayage kama ni mtu makini na mwenye nia njema kama
anavyoonekana kutaka kutushauri, angelifanya utafiti aghalab angegundua
mikakati au hatua kadhaa zinazochukuliwa na CHADEMA kujiimarisha na
kujikita katika ngazi mbalimbali kwa lengo la kuchukua dola 2015.
Je, Mayage anajua kuwa hakuna kanuni moja na inayofanana katika siasa kwa kuwa siasa “
is a game of dynamics” yaani ni mchezo wa mbinu na mikakati.
Hata hivyo, hata hao waliosema kuwa nimemtukana au kumdhalilisha Mayage, hawakueleza ni tusi gani ametukanwa.
Kutokana na mazingira hayo, nimeona nitoe ufafanuzi ufuatao.
Si mara ya kwanza
Si mara ya kwanza tunajibishana na Mayage, baada ya makala au
nyaraka zake. Kwa wale wanaokumbuka alikuwa akiandikia gazeti la Rai.
Mayage aliwahi kuandika “Waraka wa wazi kwa Dakta Slaa” katika makala
tatu mfululizo na zote zilikuwa za upotoshaji. Makala hizo zilikoma
pale nilipomjibu kupitia gazeti hilo hilo.
Katika barua zake hizo niliamini tatizo lilikuwa kutokufanya
utafiti, lakini baadaye niligundua kuwa licha ya kutofanya utafiti
Mayage alikuwa “kuwadi” wa waliomtuma kwa malengo waliyokuwa wakijua
wenyewe.
Jambo hilo alilikiri kwangu kwa
sms Mayage mwenyewe, baada
ya kuondoka Gazeti la Rai. Nami nikampongeza kwa unyofu na uwazi wake.
Kama ni mkweli na mnyofu atatoka hadharani na kukiri mawasiliano kati
yetu.
Kwa nini niliandika sms
Niliposoma makala ya Mayage katika Gazeti la
Raia Mwema, kwa kutumia saikolojia tu ya kawaida nilijua alikokuwa akielekea ndiyo maana nikamtumia
sms bila kutaka kumjibu kwenye gazeti ili ajirekebishe kabla hajafika mbali.
Kwa bahati mbaya, nia yangu njema kwa Mayage ikaanguka kwenye jiwe
gumu, badala ya kuanguka kwenye udongo wenye rutuba. Hii haikuwa kwa
bahati mbaya, kwani wakati anaanzisha safari ndefu ya makala zake
alikuwa anajua alitaka kuhitimisha vipi.
Hii imeonekana dhahiri katika makala yake ya sasa “Ombwe….mbadala wa CCM ni chama kipya”. Mengine yote ni kisingizio tu.
Hoja anazotoa kwetu
Hoja zake ni kwanza, CHADEMA ijikite zaidi katika “kufanya siasa
badala ya uanaharakati wa maandamano”. Pili, wabunge wa CHADEMA
wanatakiwa kuja na programu za maendeleo kwa wananchi wa majimbo yao
“ili yasije yakakikuta yaliyokikuta chama cha NCCR-Mageuzi..”
Tatu, katika makala yake ya wiki iliyopita yenye kichwa cha habari
“Sababu tunayo, tuwang’oe 2015”, alitoa sababu mbalimbali na hatimaye
alitoa “ushauri kwa wazalendo wenye uchungu wa kweli ….kuanzisha chama
cha siasa makini sasa, si kusubiri kesho na Watanzania wakiunge mkono
kwa nguvu zote…”
Majibu kwa hoja zake
Mimi sina tatizo na ushauri wa kuanzishwa kwa chama kipya kwa kuwa
ni haki ya kikatiba ya Watanzania. Msingi wa kumtaka Mayage kufanya
utafiti ni katika upotoshwaji dhahiri wa Mayage, ambaye kwa ufundi
mkubwa amejenga hoja kinzani (
fallacy) inayoonyesha kuwa
CHADEMA si chama makini, hakifanyi siasa makini bali kinafanya tu
uanaharakati. Huu ndio msingi na kiini cha kumtaka bwana Mayage afanye
utafiti kuhusiana na hoja zake.
Kama hoja za Mayage kutaka kianzishwe chama kipya inatokana na hoja
za Richmond, ufisadi na sasa Jairo, na kama angelikuwa makini kidogo na
kufanya utafiti kidogo tu angeligundua ni kiasi gani CHADEMA ni ‘chama
makini’ hadi kujitosa MwembeYanga, Septemba 15, mwaka 2007 na kuibua
hadharani (baada ya jitihada za kutumia Bunge kushindikana), hoja za
ufisadi wa Benki Kuu, EPA kwa ujumla wake,
Twin Tower ya Benki Kuu, Kagoda, Ufisadi kupitia Commodity Import Support (CIS) na nyingine nyingi.
Inatosha kufungua kumbukumbu rasmi za Bunge (
hansard) za mwaka 2007/2008/2009/2010. Msomaji na mfuatiliaji makini anaona wazi kupitia
hansard jinsi Dk. Slaa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CHADEMA, alivyokuwa akipigwa “
point of order” kutakiwa kufuta sehemu ya hotuba yake na Spika, bila shaka kwa lengo la kuuficha ukweli usijadiliwe bungeni.
Mayage atakumbuka jinsi Spika wa Bunge, Samuel Sitta alivyokimbilia
TBC1 na kutangaza kuwa “Nyaraka alizokuwa nazo Dokta Slaa (kuhusu
ufisadi) ni feki na kuwa anaziwakilisha polisi ashitakiwe”.
CHADEMA hatukutetereka
CHADEMA ilishikia bango bila kutetereka, pamoja na vitisho na
matusi yote hoja hizi sasa zinajulikana, taifa zima leo linajua ufisadi
mkubwa unaokumba nchi yetu katika nyanja mbalimbali.
Leo taifa nzima linaimba na kupinga ufisadi. Hii iliwezekana tu,
kwa kuwa baada ya jitihada za bungeni kushindikana CHADEMA, kwa kukodi
helkopta ilipita kwenye makao ya mikoa 12 ya Tanzania Bara na kupeleka
hoja hizo kwa wananchi, kama Mahakama Kuu kuliko zote kwa wanasiasa.
Mzunguko huo ulihitimishwa MwembeYanga kwa kutaja hadharani majina ya
mafisadi 11.
Mafisadi wengine wako kortini
Hakuna anayebisha, na hata Mayage atakubali kuwa wengine kati ya
watuhumiwa hao wa ufisadi leo wako mahakamani kwa kesi zinazohusiana
na ufisadi huo.
Mayage anasema CHADEMA kinafanya kazi “ki uanaharakati” angelifanya
utafiti kidogo tu angelijua matokeo ya uanaharakati huo kwa siasa za
CHADEMA na kwa siasa za Tanzania baada ya MwembeYanga.
Kwenye
sms niliyomtumia nilitumia neno kwa mtu yeyote anayefikia hitimisho (
conclusion)
bila utafiti ni ‘uvivu wa kufikiri’ na bado nitasimamia hapo kwa
kuwa kuacha hoja ya Mayage bila kupata majibu ya kina tutaruhusu
upotoshaji unaozidi viwango vyote.
Aidha, Mayage ameshindwa kutoa tafsiri ya neno ‘siasa’ badala yake
anaona kinachofanywa na CHADEMA ni ‘uanaharakati’ tu, na hivyo
anawashawishi “Watanzania kuanzisha chama cha siasa makini”.
Waanzishe chama makini siyo kwa kuwa chama hicho kipya kina ajenda
mpya bali kwa vile tu CHADEMA si makini na kinafanya kazi
“ki-uanaharakati”.
Mayage anashindwa kuchambua kwa kina uhusiano wa karibu sana kati ya
uanaharakati na siasa. Anashindwa kuona kuwa uanaharakati inaweza kuwa
mbinu mojawapo (wakati mwingine ya lazima) ya kufikia malengo ya
kisiasa.
Hoja ya Mayage ingekuwa na mashiko angelikuwa amepitia mikoa yote 12
ambako CHADEMA ilifanya mikutano ya hadhara (uanaharakati) na
kulishitaki Bunge kuhusiana na ufisadi wa Buzwagi, hoja ya Kabwe Zitto
iliyolifanya Bunge kumfukuza Zitto, bungeni kwa miezi takriban mine, na
kuwaeleza kinagaubaga Watanzania ni nini matokeo ya mikutano hiyo kwa
Watanzania na matokeo yake (
impact) kwa siasa za Tanzania leo. Bwana Mayage alipaswa kukumbuka msemo kuwa bila “utafiti hakuna haki ya kuzungumza”(
No Research no right to speak).
KUTOKANA na kutokufanya utafiti, Mayage ameshindwa kutambua ni
Watanzania wangapi wamejiunga kutokana na hicho anachokiita
‘uanaharakati’ wa CHADEMA, na au ni matawi mangapi yamefunguliwa
kutokana na uanaharakati huo.
Ameshindwa kuona ni maeneo mangapi ambayo kabla ya mikutano au
maandamano ya CHADEMA hayakuwa na matawi ya CHADEMA na leo si tu kuna
wanachama, bali pia matawi yenye uongozi kamili.
Ni kweli CHADEMA imekuwa ikiongoza ‘maandamano’ nchi nzima kupinga
ufisadi na aina mbalimbali za matumizi mabaya ya rasilimali za umma.
Mayage angelifanya utafiti kidogo tu angeligundua kuwa CHADEMA imefanya
kuanzia Januari, 2011 (bila kutaja ya nyuma) maandamano kwenye wilaya
za makao makuu ya mikoa 16 ya Tanzania Bara (kupitia Operation Sangara
na ziara za Katibu Mkuu) na kwenye makao makuu ya wilaya zote katika
mikoa hiyo na takriban kata zote za majimbo yote katika mikoa hiyo (
isipokuwa michache ambayo hatukufika kutokana na sababu mbalimbali kama
kuzuiwa na mvua).
Mayage angelifuata ushauri wangu wa kufanya utafiti kidogo katika
mikoa hiyo na wilaya, majimbo na kata) angeliweza kugundua ni kwa kiasi
gani CHADEMA ni makini katika mipango yake na kujikita vijijini kuliko
anavyodhani kwa kutumia “nadharia ya kuandika makala mezani”. Wakati
wa kuandika nyaraka mezani umepitwa na wakati wenzako tuko mbali zaidi
japo hatuvumi.
Ushauri wa hisia ni kama kelele za debe tupu
Mayage angelifanya utafiti mdogo tu hata ‘
sample’ yaani
maeneo machache tu yaliyochaguliwa kwa umakini, ambayo inakubalika
kisayansi makala yake na ushauri wake ungelikuwa na umuhimu mkubwa na
CHADEMA tusingesita kuuzingatia.
Ushauri usio na takwimu zozote, unaotokana na hisia binafsi,
utaalamu wa mtu kukaa tu mezani na kutoa hukumu bila kusikiliza kesi ni
sawa na debe tu linalolia kwa sauti kubwa lakini “halina kitu ndani”.
Hivyo kwa wale waliodhani nimekataa ushauri wa Mayage, naomba wawe
na utulivu niliukataa kwa kufahamu malengo yake binafsi, malengo ya
makala yake. Kabila letu la
Wairaqw tuna msemo “
kuro tsihay a gawti stahha” (tafsiri ambayo kwa Kiswahili “Mwewe mwenye mimba humtambua angali angani)”.
Mimi ni Katibu Mkuu makini
Nilijua mapema Mayage angelihitimisha kama ambavyo anahitimisha katika
Raia Mwema
la Desemba 7 hadi 13, 2011; yaani “Watanzania waanzishe chama kingine
makini” (tafsiri ya anachomaanisha Mayage ni kuwa CHADEMA si makini na
ni cha ki-uanaharakati tu).
Ningeacha kuonya katika hatua hiyo nisingelikuwa Katibu Mkuu makini,
ambaye wajibu wake daima ni kulinda maslahi ya chama chake, wanachama,
wapenzi wa chama na wananchi kwa ujumla.
Nilitimiza tu wajibu wangu kwa kumtaka afanye utafiti kabla
hajazungumzia mambo yanayohusu maslahi ya wengi. Wako wenye uwezo wa
kuchambua kwa kina na wako wanaochukua mambo yalivyoandikwa. Tuepuke
kuwapotosha angalau wale wasiofanya uchambuzi wa mambo.
Sitaki kuzungumzia madhara ya makala hizi kwa kuwa sijafanya
utafiti, lakini ni dhahiri kati ya hao anaosema Mayage wamempelekea
sms,
kama hawakuwa na malengo mengine kama nilivyoonyesha awali, basi
hawakufanya uchambuzi wa kina, hawakujua pa kupata taarifa sahihi za
chama.
Bila shaka wameamini hakuna mipango wala mikakati yoyote ya kujenga
chama katika ngazi zote isipokuwa ni maandamano tu. Mayage
angelifanya utafiti angeliwaelimisha angalau kuhusu waraka wa Katibu
Mkuu na moja wa mwaka 2011, waraka na mbili wa mwaka 2011.
Waraka namba moja ambao uko katika hatua mbalimbali za utekelezaji
kuanzia wilaya, majimbo, kata na matawi. Waraka huu ulitolewa takriban
miezi mitano iliyopita kabla Mayage hajafikiria kuandika makala zake
katika
Raia Mwema kuhusu mada hii.
Angelifanya utafiti angeligundua kuwa Oparesheni Sangara zote huishia kwa kuzindua matawi na kusimika uongozi.
Utafiti ungelimwezesha Mayage kuwa na uwezo, uhalali na haki ya
kushauri Watanzania wanaopenda kuanzisha chama kingine ambacho wao
wanadhani kwa mtazamo wao ni makini.
Madhara ya kutofanya utafiti
Kukosekana kwa utafiti kunamnyima uwezo, uhalali na haki hiyo, kwa
kuwa ni hatari sana kufanyia uamuzi wa kitaifa kwa misingi ya hisia tu
ya mtu fulani bila kujali nafasi yake. Kuanzisha chama kipya ni haki
yao.
Lakini haki hiyo isitumike kumdhalilisha mwingine kwa misingi isiyo
sahihi. Dhamira hiyo ni tofauti kabisa na kutaka kianzishwe chama
kingine makini kwa kuwa CHADEMA ni cha ki-uanaharakati na kwa tafsiri
yake, si makini.
Chama hakiwi makini kwa kuwa tu mtu mmoja au kundi fulani wanadhani
hivyo na au hawafahamu mipango na mikakati ya chama hicho. Fikra hizi
ndizo zinazoitwa “
fallacious” katika falsafa.
CHADEMA hatukatai ushauri
CHADEMA hatujakataa hata siku moja ushauri wa mtu yeyote. Tumekuwa
na tutaendelea kupokea ushauri wa Watanzania wote bila kujali itikadi
zao, dini zao, wanakotoka, umri wao, jinsia zao.
Tumekuwa tukipokea ushauri kutoka kwa mtu mmoja mmoja kwenye matawi
na kwa viongozi ngazi zote. Huu ni utamaduni wa CHADEMA na Watanzania
wengi wanajua hivyo. Ushauri ukitolewa utafanyiwa kazi kama
inavyotakiwa.
Lakini upotoshwaji wa dhahiri pia unafanyiwa kazi, tena bila unafiki
kwa kuwa ndani ya CHADEMA hatujazoea unafiki wala kudanganyana; “
We shall call a spade a spade”, ndiyo maana Mayage alishauriwa afanye utafiti ili ushauri wake uwe na tija na maana kwetu na kwa Watanzania.
Tungeliweza kunyamaza bila kumjulisha, lakini angeendelea kupotosha
bila kufahamu madhara ya upotoshwaji wake. Aidha hatua niliyochukua ya
kumjulisha imeanzisha mjadala mpana zaidi na sasa nina fursa ya kutoa
ufafanuzi wa kina jambo ambalo lisingelitokea ningelimnyamazia.
Ni kweli kila mtu ana uhuru wa kufikiri na kuandika anavyotaka ndani
ya misingi ya sheria za nchi. Lakini kwa mwandishi kusema
“….nawaomba Watanzania tutoke nje ya ofisi au nyumba zetu kwenda kwa
wananchi wenzetu tuwaulize vyama hivyo vinasimamia itikadi au sera
gani…” hiki ndicho nilichomtaka Mayage atoke ofisini kwake kwanza aende
kwa wananchi kabla yeye mwenyewe hajawaambia Watanzania wengine.
Yeye anawaandikia Watanzania ambao miezi takriban 11 tu iliyopita
walionyesha mwelekeo wao kupitia kura (pamoja na hujuma zote
zilizofanyika). Sasa nani atoke kwa wananchi, Mayage au wananchi ambao
kimsingi siyo tu wanajua wanachotaka, bali wamekwisha kuonyesha kwa
matendo.
Nina hakika Mayage angeenda na swali lake; “ni chama gani
kimesimamia kwa ustadi hoja yake ya kuwakomboa Watanzania kutoka
mikononi mwa madhila ya CCM..” angepata jibu la Watanzania na si
kupotosha kama anavyoelekea kuwashawishi kuanzisha chama ambacho
hawajakiona, hawajafanya kazi nacho na hawakijui.
Ni kwa nini Mayage atake Watanzania wawe watu wa kufanya majaribio
kila wakati? Ni kwa sababu tu yeye kajibiwa vibaya kama anavyosema na
Dk. Slaa au kuna sababu nyingine?
Kama ni kweli katukanwa na Dk. Slaa ni kwa vipi anaihusisha CHADEMA
yote, kwani hafahamu kuwa leo CHADEMA si Mbowe, si Slaa wala viongozi
bali ni taasisi ya Watanzania wenyewe.
Msingi wa mvutano umeya Arusha
Mayage anasema CHADEMA wanalumbana kuhusu umeya wa Arusha!
Angekuwa makini angelitafuta misingi ya mgogoro. Amewauliza watu wa
Arusha?
Kama hajafanya utafiti ana uhalali gani kuwasemea watu wa Arusha
ambao wanajua wanalofanya kwa kuambatana na mbunge wao ambaye
alidhalilishwa ubinadamu wake na ubunge wake katika uchaguzi wa meya
Arusha.
Ni ulimbukeni kufikiri mtu anajua kwa kuandika tu kutoka mezani.
Hiki ndicho walichofikiri madiwani watano wa CHADEMA waliotaka kutikisa
kiberiti. Walishindwa kusoma alama za nyakati kama alivyo Mayage.
Mayage anaamini na ‘kusingizia’ CHADEMA inapigania kupata umeya, hajui kuwa CHADEMA inapigania misingi “
principle” na si vinginevyo.
Tofauti ni kubwa sana baina ya mawili hayo. CHADEMA imesimamia hoja yake yaani “taratibu za uchaguzi wa meya zimekiukwa.”
Uongozi wa CHADEMA haukuwa tayari kuona taratibu na sheria
zinavunjwa na wanaotarajiwa kuzilinda, yaani Serikali. Hii haina maana
ya kuwa CHADEMA inataka meya atoke CHADEMA kama anavyotaka ieleweke
Mayage. La hasha.
Hili nalo ni tunda la kutojua misingi ya jambo na kudandia hoja kwa kuwa tu ana fursa ya kuandika makala mezani.
Mayage angelifanya utafiti angeligundua hoja ya Katiba mpya ilikuwa
ndani ya Ilani ya CHADEMA. CCM imeibeba baada ya kushinda uchaguzi kama
walishinda na siyo ‘kuiba kura’ (Katiba hairuhusu kuhoji matokeo hivyo
hatuna pa kutolea ushahidi wetu). Sisi hatuna shida na hilo.
Tunasisitiza kama wamechukua hoja ambayo hawakuwa nayo waitekeleze
vizuri kama ilivyobuniwa na walioibuni. CHADEMA ndiyo iliyoibuni, na
kusema...“
ndani ya siku 100 mchakato wa Katiba mpya utaanza” Hakuna chama kingine chochote kilichosema hivyo kwenye ilani yake.
Ni dhahiri Mayage haelewi, kuwa ‘Mchakato ukiwa mbovu, tunda lake
yaani Katiba itakayopatikana itakuwa mbovu’. Wengine tuna uzoefu si wa
kusoma tu magazetini bali kushiriki mchakato wa Tume ya Rais ya Jaji
Kisanga. Ni hovyo. Ndiyo maana tangu siku ya kwanza nimepinga Tume ya
Rais badala ya Tume ya Wananchi itakayoundwa na mkutano wa Katiba.
Mayage haelewi kuwa uchaguzi unaendeshwa kwa Katiba na kuwa haki
haitapatikana kama Katiba itaendelea kubeba Chama cha Mapinduzi (CCM).
Ni ndoto kufikiria uchaguzi huru na haki 2015 kama Katiba Mpya
haitapatikana. Matukio yote ya wananchi kupigwa mabomu, kuzuiliwa
mikutano ya upinzani mara kwa mara, kubadilishwa kwa matokeo ya
uchaguzi yote haya ni matokeo ya Katiba mbovu.
Mayage hajui kuwa migogoro mingi kwenye ardhi ni matokeo ya Katiba
mbovu! Hajui kuwa robo tatu ya bajeti ya taifa leo inatumika kwenye
uendeshaji wa Serikali badala ya mipango ya maendeleo kutokana na
Katiba mbovu? Mayage siyo tu hajafanya utafiti, lakini pia si makini
katika kujenga hoja zake. Anajipinga mwenyewe mara aseme chama gani
kimesimamia hoja zake, mara aseme CHADEMA kinapoteza muda kujadili hoja
zenye manufaa kwa Watanzania. Tumuamini kwa lipi katika hali hii?
Mayage sisi tuliisha kumaliza utafiti na udadisi kuhusu Katiba.
Huhitaji kwenda mbali, nenda Ghana na Kenya. Tunayo michakato
iliyotumika kupata Katiba na tunazo pia nakala za Katiba zao.
Nani kapotea kati yako wewe ambaye huna hata mfano mmoja na CHADEMA
inayofahamu tangu awali nini kinahitajika kupata Katiba mpya!
Tuache ulimbukeni tunapozungumzia maslahi ya taifa. Mayage anaenda
mbali kiasi cha kufananisha CHADEMA na “bundi katika msafara wa ndege
dhaifu”! Kama yeye alijisikia kutukanwa je, na CHADEMA ambaye si mtu
mmoja inajisikiaje na upotoshwaji na matusi ya kiasi hiki?
Ukisoma kwa umakini, kwake Mayage CHADEMA ni “chama cha ovyo” ndiyo
maana anawashawishi Watanzania kuanzisha chama mbadala wa CCM.
Mayage amelundika vyama vyote 17 vya upinzani katika kapu moja. Ni
kweli kuwa hafahamu CHADEMA ni chama pekee cha upinzani kinachoongoza
halmashauri zaidi ya saba? Hajui kuwa CHADEMA imeshindwa kwa idadi
ndogo sana katika halmashauri nyingine nane?
Mayage ameshindwa kutambua kuwa CHADEMA ni chama kinachokua
kimkakati na vigezo ni vingi chukua idadi ya madiwani ambayo katika
uchaguzi wa 2010 imeongeza kwa asilimia zaidi ya 400, mafanikio ambayo
hakuna hata chama chochote cha upinzani kimefikia?
Mayage hajui kuwa katika vyama 17 viko ambavyo tangu vianzishwe
havijawahi kupata kiongozi hata serikali moja ya mitaa angalau
mwenyekiti wa kitongoji, wakati CHADEMA ina maelfu ya viongozi hao?,
Mayage ameamua kuzipuuza makusudi kwa malengo anayojua na pia kwa ‘uvivu
wa kutokufanya utafiti’ angalau kupiga simu tu kwa wahusika. Madhara
yake ni kuwaambia watanzania “..tulivyonavyo sasa (vyama vya
siasa/NGO’s). Hivi haoni hata aibu kulinganisha chama kinachoongoza
halmashauri zikiwemo Jiji la Mwanza na NGO ambayo malengo yao si
kuchukua dola?
Haya siyo matusi tu kwa Watanzania bali kwake mwenyewe aliyejifanya
mtaalamu akashindwa kufikisha ujumbe ambao pengine hata mtoto wa shule
ya msingi angeliweza kuufikisha vizuri zaidi.
Wanachama,wapenzi na Watanzania wapenda mabadiliko ambao walikuwa
hawajagundua dhamira ya Mayage kuanzia makala ya kwanza ni vema
wakarudi kusoma makala zake za mwanzo na kuzichambua kwa kina ili
kuepuka upotosha uliojificha kwa hoja za kuuma na kupuliza.
Dk. Slaa nisingeliweza kwa namna yoyote kufumbia macho upotoshwaji huu ambao nia na lengo lake ni dhahiri.
Mayage anaonyesha udhaifu mkubwa pale anaposema hajaridhishwa na
CHADEMA kwa kushindwa kusimamia hoja moja tu “…ya posho ya vikao kwa
wabunge”. Kwani CHADEMA ndiyo inayolipa posho hiyo?
Hajui mgogoro wa sasa wa posho kulipwa kinyemela na jinsi CHADEMA
kama chama inavyopiga kelele, hajui jinsi CHADEMA ilivyodai fomu ya
mahudhurio ukumbini bungeni itenganishwe na fomu ya posho, na uongozi
wa Bunge umekataa kufanya hivyo?
Labda hajui msimamo wa CHADEMA kwa kuwa si mpenda kusoma wala hajui
ilani ya CHADEMA kifungu cha 5.5.1 (2 na 6) ya Agosti 2010, kinasema
nini.
Lakini sishangai kwa vile anaandika kwa hisia badala ya utafiti.
Kama ambavyo hajui pia kuwa kamati kuu ya CHADEMA kila kikao kwa mujibu
wa kanuni, inatakiwa kupokea utekelezaji wa programu ya kazi kutoka
kwa wabunge na halmashauri zinazoongozwa na CHADEMA na kila kamati
tendaji ya kata inapokea taarifa ya utekelezaji kutoka kwa madiwani
wake.
Inawezekana utekelezaji wa mipango katika maeneo yanayoongozwa na CHADEMA unasua sua na kwa maeneo mengine hauridhishi.
Lakini pia angetafiti kidogo angegundua halmashauri zenye uzoefu za
CHADEMA zimepiga hatua kiasi cha kuanzisha chuo chake cha waalimu
kupunguza kero ya upungufu wa waalimu, kuanzisha chuo cha madaktari
(clinical officers) na manesi kupunguza kero ya upungufu wa wataalamu
hao na sasa wako mbioni kuanzisha chuo cha kilimo.
Haya yanapatikana tu kwa wenye nia na dhamira ya dhati ya kutaka kujua bila kutoa hukumu mezani.
RC Mwanza, ma-DC wametuhujumu
Angelifanya utafiti angeligundua jinsi mkuu wa mkoa wa Mwanza
alivyoingilia na kuvuruga utekelezaji wa mipango ya Jiji la Mwanza
iliyoko chini ya CHADEMA, na vivyo hivyo kwa wakuu wilaya katika
halmashauri zingine.
Utafiti ungelimwonyesha kuwa demokrasia kwa wengi wa viongozi wa
Serikali iko kwenye midomo zaidi (lip service) lakini yanayoendelea
maeneo mengi nchini ni kinyume cha demokrasia. Haya hutayajua kama huna
dhamira ya kutaka kuyajua na wala hufanyi utafiti. Ndiyo msingi mkubwa
wa ushauri wangu kwa Mayage.
Ni dhahiri Mayage angelifanya utafiti angeligundua maandamano
yalivyowaunganisha Watanzania kudai siyo tu haki zao mbalimbali, bali
kupaza sauti yao dhidi ya makali ya maisha kama vile sukari, bei ya
sembe, mafuta ya kupikia, mafuta ya taa pamoja na kuwakatalia watawala
kodi yao isitumike kulipa madeni ya Dowans..
CCM wameiga hawakufanikiwa
Anachokiita Mayage uanaharakati, angelijikita kwenye utafiti
angeligundua matokeo yake ni nini hadi CCM wenyewe waliokuwa wakikandia
maandamano wakaamua kuyaiga walipojaribu kuandamana Mbeya japo
hayakufanikiwa.
Ni dhahiri Mayage amejikita kwenye mbinu mgando akidhani namna pekee ya kufanya siasa ni kufungua matawi kwa mtindo wa CCM.
Kwa kuwa hajafanya utafiti anashindwa kugundua kuwa mbinu za CCM za
kufungua matawi haziwezi kufuatwa na chama kingine chochote makini kwa
kuwa CCM inatumia mfumo wa dola kufanya kazi zake-watendaji wa vijiji,
kata, makatibu tarafa, wakuu wa mikoa, wilaya, kwa ujumla mfumo mzima
wa Serikali.
Polisi wanaingilia mipango yetu
Angetafiti angeligundua hata matawi niliyofungua au kufanya
yafunguliwe kutokana na ziara ya Katibu Mkuu Jimbo la Mbinga Magharibi
(Mbamba Bay), bendera zote zimeshushwa kwa amri ya OCD.
Angelikuwa mtafiti angeligundua chama makini kama CHADEMA
kinakumbana na matatizo na vikwazo gani. Angelitoa ushauri jinsi ya
kupambana na changamoto hizo nisingelikuwa na sababu ya kumjibu Mayage
na au ningemjibu kwa kumpongeza.
Ushauri wake ungetokana na utafiti nina hakika ungewasaidia sana kuwafungua macho Watanzania badala ya kuwapotosha.
Kauli ya Mayage kuwa ‘..Ndani ya siasa wako wanasiasa wazuri tu,
lakini hao hawana sauti wala nafasi ya kukielekeza chama hicho…wenye
sauti na ushawishi ndani ya chama ni wanaharakati hali inayokifanya
chama kiendeshwe kiharakati kwa asilimia 80..” inathibitisha siyo tu
Mayage hajafanya utafiti, lakini pia hajui ‘ABC’ ya siasa na hivyo
hastahili kuandikia hata mada za kisiasa.
Chama cha siasa hakiendeshwi kwa ‘influence’, au uanaharakati kama
anavyodai Mayage bali na Katiba, kanuni na taratibu za ndani ya chama
husika kama zipo.
Kwa faida ya wapenzi wa CHADEMA na Watanzania kwa ujumla CHADEMA
inaendeshwa misingi ya Katiba yake, na toleo la mwisho ni la mwaka
2006. CHADEMA ni kati ya vyama vichache vyenye kanuni za uendeshaji,
maadili ya viongozi na wanachama, kanuni za uendeshaji wa halmashauri
zinazoongozwa na na CHADEMA ikiwa ni pamoja na serikali za mitaa
zilizoko chini ya CHADEMA na hatimaye kanuni za nidhamu ikiwa ni pamoja
na kanuni za nidhamu za wabunge, madiwani, na wenyeviti wa serikali za
mitaa (na wajumbe wao).
Uamuzi wa CHADEMA hufanywa kupitia Sekretariati ya Kamati Kuu ya
chama, Kamati Kuu, Baraza Kuu na mkutano mkuu ambacho ndicho chombo
kikuu na cha mwisho cha uamuzi.
Je, ni kuwadi wa maadui zetu?
Kwamba CHADEMA inaendeshwa na wenye ‘influence’ ni kielelezo cha
kile nilichokisema kuwa kauli kama hizo zinatoka tu kwa watu wenye
uvivu wa kufikiri na kufanya utafiti.
Vinginevyo Mayage ana ajenda yake ambayo hajaiweka hadharani na au ni kuwadi tu wa maadui wengi wa CHADEMA.
Kama nia yake ni njema kama anavyotaka kuonyesha na kuwa anatoa
ushauri kwa nia njema, huwezi kumshauri mtu usiyemfahamu, na huwezi
kumfahamu mtu kama angalau humtembelei, kumjulia hali, kuomba nyaraka
zake na kadhalika.
Wakati ninawapokea waandishi wengi na wa vyombo takriban vyote
ofisini kwangu Mayage hajakanyaga wala hajaomba taarifa yoyote iwe kwa
simu iwe kwa mahojiano. Huu ni uthibitisho kuwa Mayage ana ajenda zake
anazozijua.
Kwa taratibu hizi uanaharakati na “influence” inapata wapi nafasi?
Au Mayage anataka kufanya kazi kwa mapenzi ya mtu mmoja mmoja mathalan
hiyo asilimia 20 anayoisema?
Je, ni kweli kuwa hiyo influence imepenya kwenye ngazi zote kuanzia
sekretariati, kamati kuu, baraza kuu hadi mkutano mkuu. Kama hivyo
ndivyo si ndivyo pia jina letu linavyodhihirisha Chama cha Demokrasia
na Maendeleo?
Au Mayage anataka tukiuke misingi ya demokrasia na asilimia 80 ya
viongozi waongozwe na asilimia 20? Huo ni ulimbukeni katika siasa na
itakuwa ni mfumo mpya unaobuniwa na Mayage katika chama chake kipya
anachosema kitakuwa makini”.
Wapenzi na Watanzania kwa ujumla hakuna sababu ya kuwa na hofu na
watu wa aina hii, na kwa taarifa yenu wako wengi wasiotutakia mema.
Naamini ufafanuzi huu wa kina utakuwa umewatoa wote hofu wale waliokuwa na shaka baada ya kusoma makala za Mayage.
Naomba nirudie tena katika hitimisho, sina tatizo na wale wote wenye
nia ya kuanzisha chama kingine kipya akiwemo Mayage kama nilivyosema
ni haki yao ya kikatiba.
Kwa wale ambao tumekwisha kuanza safari ya kuing’oa CCM kupitia
‘meli yetu’ ya CHADEMA, tuendelee na mikakati yetu na kila mmoja
akitimiza wajibu wake, Novemba 2015 CCM itaingia kwenye kumbukumbu ya
historia kama ilivyo UNIP (Zambia) na KANU (Kenya), tena vyote ni vyama
vinavyojulikana kama vyama vya ukombozi.
Mwalimu aliwahi kusema “play your part, it can be done” kila
kiongozi wa CHADEMA kwenye ngazi na nafasi yake atimize wajibu wake na
apuuze propaganda za maadui zetu zikiwemo hizi za Mayage.