Tuesday, November 6, 2012

SHERIA 10 ZA J.ULIMWENGU KUHUSU ELIMU

Rai ya Jenerali

Jenerali Ulimwengu
Toleo la 058
3 Dec 2008
KATIKA makala zangu za nyuma nimekwisha kubainisha baadhi ya mambo ninayoamini kwamba ni muhimu katika kujenga elimu itakayoikomboa nchi yetu na watu wake kutoka kwenye umasikini kuelekea kwenye maendeleo.
Nimeonyesha jinsi ambavyo mipangilio yetu ni mibovu katika maeneo kadhaa, na nimetoa rai kwamba elimu tunayotoa kwa watoto wetu haiwezi kuwakomboa wala kuliendeleza Taifa letu.
Ukweli ni kwamba elimu yetu ni kivuli hafifu cha elimu ya kikoloni; imekosa ‘ubora’ uliokuwa ndani ya elimu ya kikoloni ya wakati ule na pia imekosa maudhui ya kiukombozi kwa sababu haionekani kuwa na malengo thabiti yanayoangalia mustakabali wa nchi yetu. Katikati ya vigoda viwili, elimu yetu imedondoka sakafuni.
Kwa bahati mbaya, tumezoea kuona mambo yanakwenda mrama katika nyanja mbali mbali na kudhania kwamba yatajirekebisha yenyewe bila juhudi zetu. Sana sana tutayagusa kidogo na kuyatomasatomasa lakini mwisho wa siku tunayaacha yalivyo tukitaraji kwamba yatachoka yaondoke.
Tumekataa kukubali kwamba mfumo mzima wa elimu yetu umevurugika, na badala ya kukubali kwamba turudi katika chumba cha usanifu na kuuchora mfumo huo upya, tunahangaika kujenga vyumba vingi zaidi vya kueneza ujinga kwa gharama kubwa.
Kinachohitajika katika mfumo wa elimu yetu si jambo jingine bali ni Mapinduzi ya Elimu ambayo itaandamana na Elimu ya Mapinduzi itakayozagaa katika sekta nyingine zote muhimu. Hii ni kwa sababu, tutake tusitake, sekta kadhaa muhimu nazo zina taswira ile ile tunayoiona katika elimu.
Ndiyo maana, kama sehemu ya majumuisho, napendekeza mambo kadhaa ambayo naamini hatuna budi kuyazingatia iwapo tunataka kuleta mapinduzi ya kweli na kuifanya elimu yetu iwatumikie watu wetu.
MOJA: Tuwatendee haki walio wengi, ambao tunajua kwamba hawataingia katika vyuo vya elimu ya juu. Nimekwisha kuonyesha jinsi ambavyo ni kijisehemu kidogo sana cha watoto wanaoingia shule ya msingi watakaoweza kuendelea hadi chuo kikuu, ni uonevu na kwa kweli na aina fulani ya wizi, kuwekeza katika elimu ya akademiki itakayowasaidia hao wachache na kuwaacha walio wengi hawajui kinachoendelea.
PILI: Kutokana na MOJA hapo juu, tujenge mfumo wa elimu na mitaala itakayowafanya watoto wa nchi hii wawe na manufaa kwa jamii zao kwa kuwafundisha njia bora za kuinua na kuendeleza uchumi wa familia zao. Watoto wa wakulima wafundishwe kilimo bora; watoto wa wafugaji wajifunze ufugaji bora, na kadhalika.
TATU: Tuache kujidanganya kwamba tunaweza kuwafundisha watoto wetu na wakaweza kuleta mapinduzi ya sayansi na teknolojia kwa kutumia lugha wasiyoielewa na isiyoeleweka hata kwa waalimu wao.
Watoto wafundishwe Kiingereza kama lugha, pamoja na lugha nyingine za kigeni, na lugha hizo zifundishwe kwa ufasaha mkubwa, lakini tusidhani kwamba hata siku moja tunaweza kumiliki sayansi na teknolojia kwa kutumia lugha isiyozungumzwa na wananchi walio wengi. Hili halijatokea kokote duniani, na sielewi ni kwa nini tunaamini kwamba litaanzia kwetu.
Tuangalie pia ni kwa jinsi gani katika maeneo fulani fulani tunaweza kuzitumia lugha zetu za asili katika elimu ya awali ili kuwapunguzia mikanganyiko inayowapata wanapoanzia na lugha wasiyoizungumza nyumbani.
NNE: Shule ni sehemu mojawapo muhimu katika kujenga ujamii (‘socialisation’). Ni mahali ambapo watoto hupikwa na kukuzwa katika maadili ya utaifa, umoja, upendo na kadhalika.
Mifumo ya elimu inayotofautiana katika nchi moja inabeba hatari ya kuzalisha makundi yanayosigana sana katika mitazamo yao ; ipo hatari ya kweli ya kuwa na makundi ya wateule waliopata elimu ‘bora’ na wanaozungumza lugha ya kigeni na Kiswahili chao ni cha wasiwasi, na makundi ya watoto wenye elimu ya hovyo na wasioweza kuzungumza Kiingereza wala Kiswahili, wala lugha za mama zao.
TANO : Kutokana na NNE hapo juu, tuwekeze kwa dhati, kwa kutenga rasilimali za kutosha na kuwekeza katika tafakuri ya pamoja, katika shule za umma, kuzifanya ziwe na ubora wa hali ya juu kiasi kwamba isiwepo haja ya wazazi kutaka kuwapeleka watoto wao katika shule binafsi. Hivi ndivyo ilivyokuwa huko nyuma wakati kila mzazi alipenda mtoto wake aende shule ya serikali, kusoma katika shule binafsi ilikuwa ni ishara ya udhaifu.
SITA : Shule ifundishe sayansi, hisabati  na lugha. Lakini pia ifundishe maadili mema ili kujenga raia wema. Sayansi, teknolojia, hisabati na lugha ni nyenzo muhimu katika makuzi ya kijana, lakini iwapo nyenzo hizo hazitaambatana na mafunzo na malezi yanayolenga uungwana ipo hatari kwamba hao vijana wanaopata elimu hiyo watazitumia nyenzo hizo katika uhalifu.
SABA: Watoto wafundishwe na watiwe shime ya kufanya tafakuri ya kiudodosi (‘critical thinking’). Elimu ya kimapokeo tuliyopewa sisi wa rika langu ilijali sana ukusanyaji wa maarifa ya kila aina na kuyahifadhi kichwani ili ‘kuyatapika’ pindi unapokuja mtihani. Hivyo, tulimezeshwa tani na tani za taarifa, na bila shaka hii ilidhoofisha uwezo wetu wa uchambuzi kwa kiwango fulani.
Leo hii hali imebadilika mno kwa maana kwamba taarifa zinaweza kupatikana kwa urahisi wakati wo wote zinapohitajika, kutokana na ukuaji wa kasi kubwa wa teknolojia. Tovuti inamwezesha ye yote anayetaka kupata taarifa kutoka kila pembe ya dunia, alimradi mtu ajue anataka taarifa gani na jinsi ya kuzipata.
Jambo muhimu sasa ni kujua ni taarifa gani tunahitaji, namna ya kuzipata na jinsi ya kuzichakata ili ziwe za manufaa kwa mtumiaji. Katika hili ‘critical thinking’ ni muhimu sana kwa sababu ndiyo nyenzo kuu ya uchambuzi, na bila uchambuzi hakuna maendeleo.
Aidha, vijana wa Tanzania wafundishwe kujiamini, kutafakari na kusema kwa sauti kile wanachokiamini. Jamiii yetu imejaa watu wenye uwezo mkubwa lakini ambao wamezoezwa kutosema wanachokiamini, na matokeo yake ni kwamba wale wanaothubutu wanalazimisha kupitisha maoni yao hata kama mawazo yao hayana maana.
Ubishi si lazima kiwe kitu kibaya, kama unatumika kwa manufaa ya jamii, hususan pale jamii inapokuwa imezama katika imani za kijinga. Socrates alikuwa mbishi na Galileo pia. Wa kwanza aliuawa, wa pili akalazimishwa kukana utafiti wake. Leo tunatambua mchango uliotokana na ‘ubishi’ wao.
NANE: Pamoja na maadili, watoto pia wafundishwe kupenda vitu vizuri, ikiwa ni pamoja na umaridadi, michezo, sanaa, ikiwa ni pamoja na muziki na ushairi kama sehemu ya ujenzi wa jamii ya watu wanaopenda mazingira na wanaoishi maisha ya siha na furaha. Elimu inayomfunza mtoto hisabati lakini haimfundishi namna ya kuvaa vizuri, kula kwa staha na kuongea kwa ufasaha katika lugha inayoheshimu hadhira inaunda roboti, si binadamu.
TISA: Suala la ubora wa waalimu liwe nambari moja kwa sababu bila waalimu bora yote mengine tunayoyafanya, kama vile ujenzi wa majumba na kadhalika, ni upuuzi. Waalimu watokane na wahitimu wenye ubora wa juu kuliko wengine; watambulike kwa uwezo wao mkubwa katika msomo yao; waandaliwe vyema na walipwe mishahara mizuri na wapewe marupurupu wanayostahili.
Turudishe heshima na hadhi aliyokuwa nayo mwalimu siku za nyuma, kwa kutambua kwamba ubora wa nchi yo yote utalingana na ubora wa mwalimu wa mwisho wa nchi husika.
KUMI: Tuuchunguze upya muda wa mafunzo ya awali. Binafsi naamini kwamba miaka saba haitoshi kumwandaa kijana kuwa wa manufaa kwake mwenyewe au jamii yake. Anapomaliza shule baada ya shule ya msingi anakuwa bado ni mdogo sana na, kwa mitaala ya sasa, hana ujuzi wo wote wa maana wa kumsaidia kujikimu.
Miaka tisa au 10 itampa kijana muda wa kuweza kujifunza stadi za kazi, ambazo anaweza kuzinoa anapoingia katika chuo cha VETA, au hata asipokwenda VETA zikamwezesha kufanya kazi moja kwa moja.
Hizo ndizo ‘sheria’ zangu 10, ambazo naamini zinaweza kuongezwa hadi kufikia 100. Hebu tuzijadili.

No comments:

Post a Comment