Tuesday, November 6, 2012

Tukatae ‘bantu education’

Rai ya Jenerali

Jenerali Ulimwengu
Toleo la 066
28 Jan 2009
NAAMINI kwamba nimetumia muda wa kuridhisha na nafasi ya kutosha kujadili umuhimu wa kuwekeza katika kuwajenga wananchi kiakili na kimwili, mkazo ukiwa katika uwekezaji unaowalenga watoto wa Taifa hili.
Bila shaka hivi ni vipengele vya mjadala vitakavyorejewa kila mara, washiriki tukiwa ni sote tunaoona haja ya kukusanya mawazo yetu na kuyachakata kwa pamoja ili tujenge mwafaka kuhusu mambo muhimu yanayotuhusu.
Tusipofanya mjadala wa dhati tutaendelea kulalamika bila ye yote kutoa maoni juu ya namna ambavyo tunaweza kujikomboa kutoka katika umasikini unaozidi kuwakandamiza watu wetu ambao wamerithishwa nchi tajiri lakini hali zao hazifanani kabisa na utajiri huo.
Tusipoingia katika mchakato wa kweli juu ya masuala yanayohusu kuondoa umasikini na tukajifunza kwamba haya mambo si ya kupapukia bali hupangwa, tutaendelea kufukuzana na wananchi tukiwadai michango ya shule ya kujenga shule zisizo na waalimu wala vitabu; watatuona kama maadui zao wakati sisi tukijidanganya kwamba tunawapelekea ‘maendeleo’.
Bado zinatufikia taarifa za watu wanaokimbia kaya zao ili wasikamatwe kwa kushindwa (au kutokutaka) kulipa michango ya kujenga ‘madarasa.’ Baadhi yao wanaweza wakawa ni watu ambao kwa kweli kabisa hawana uwezo wa kulipa ‘michango’ hiyo, lakini baadhi yao wanaweza kuwa wale ambao, hata kama wanao uwezo wa kutoa fedha, hawaoni faida yo yote inayopatikana na ‘elimu’ inayotolewa ndani ya majumba yasiyo na walimu wala vitabu.
Kinachowafanya watendaji wa maeneo ya vijijini wawasake wananchi kama wahalifu ni maelekezo wanayopewa kutoka kwa waajiri wao wa Dar es Salaam, ambao katika mantiki ambayo inazidi kupinda kila uchao, bado wanaamini kwamba elimu ni sawa na idadi ya vyumba vya tofali na bati.
Maelezo yote yaliyotolewa na wataalamu kuhusu maana halisi ya elimu yamepuuzwa, na shughuli ya kuwahangaisha wananchi inaendelea mtindo mmoja.
Nimemuuliza rafiki yangu mmoja ambaye alikuwa kijijini katika kipindi cha Noeli na Mwaka Mpya ni kwa nini basi msisitizo huu wa ujenzi wa majengo yasiyokuwa na maana haujajulikana kwa wakuu wa nchi; jibu lake ni kwamba wanajua lakini hawajui wafanye nini  kwa sababu walikwisha kuagiza ujenzi ufanyike, na kwa hiyo ujenzi ni lazima ufanyike, na wazee wa kijijini wanaziona hizo ‘shule’ kama vituo vya kuwachunga watoto wa kike wasipate mimba!
Ipo mizaha inayovumilika, lakini huu si aina mojawapo ya mizaha hiyo. Huku ni kucheza na maisha ya watu na ni hatari kwa mustakabali wa Taifa. Siamini kwamba watu wetu wataendelea kuwa wa kusema “E walla” siku zote wakati wanaona mambo yanayofanyika yanawaumiza na kuwafanya watoto wao wasiwe na tumaini angalau la kuweza kuyafanya maisha yao yawe bora kuliko ya wazazi wao.
Hebu tukumbushane tena ( na kwa wale wasio na hadhi ya kukumbuka, kwa sababu hawajawahi kulisikia hili, tuelimishane) katika mambo yote unayoweza kuyafanya kwa ajili ya watoto wako hakuna hata moja linaloweza kulinganishwa na elimu bora na afya njema. Mengine yote yanakuja baadaye.
Kilicho dhahiri ni kwamba watawala wetu ni wazazi pia, na tunaona jinsi wanavyohangaikia elimu na afya za watoto wao. Kwamba hawahangaikii elimu na afya za watoto wa jamii za kimasikini si kwa sababu hawajui umuhimu wake; ni ubinafsi. Nafasi walizo nazo zingeweza kuwapa fursa ya kutumikia wananchi wa matabaka yote, na kwa kufanya hivyo tukapunguza ukali wa mapambano ya kitabaka katika siku zijazo.
Haitusaidii kupoza ghadhabu za wanyonge wanaoona watoto wao wanapewa ‘elimu’ inayofanana na ile iliyoitwa ‘bantu education’ wakati wa utawala wa Makaburu Afrika Kusini, huku watoto wa wakubwa wanapewa kila aina ya fursa, nchini na ughaibuni. Siku moja watalikataa hili… mwenye masikio na asikie.
Aidha, haiwezekani kwamba katika mazingira ya mijadala inayoendelea nchini kuhusu ‘ufisadi’ kwamba wananchi hawatajaribu kuuunganisha huo ‘ufisadi’ na hali zao mbaya za maisha na mifumo inayoonekana kutaka kumlaani mtoto wa mtu wa chini ili asiweze hata siku moja kusimama kwa miguu yake mwenyewe.
Mzee mmoja kutoka Kanda ya Ziwa ameniambia jambo ambalo siwezi kulisahau: Mtoto anapelekwa shule akiwa na miaka saba; anakaa huko kwa kipindi cha miaka 7; ‘anamaliza shule akiwa na miaka 14; shule hakuweza kujifunza hata huo ujuzi wa kusoma na kuandika, na nyumbani hakuwapo kujifunza namna ya kutunza ng’ombe na kulima pamba; kwa hiyo huku hayuko na kule hayuko.
Sasa mzee kama huyu unampa jibu gani anapokuambia kwamba yeye anatoa ‘kitu kidogo’ ili afisa elimu na wale watendaji wanaokuja kuswaga watoto kuwapeleka ‘shule’ wairuke kaya yake kama isiyokuwa na mtoto wa umri wa kwenda shule. Kwa kufanya hivyo angalau mtoto atabaki nyumbani ajifunze kuchunga ng’ombe!
Yote haya yana maana kwamba hatuna budi kujiwekea utaratibu wa kujadiliana kwa pamoja kuhusu hatua zote za maendeleo tunazokusudia kuzichukua. Tabia ya watawala wa nchi hii, na wa Afrika kwa ujumla, ya kufanya mambo wanavyotaka wenyewe imekuwa ni kikwazo kikubwa mno katika maendeleo ya nchi hii na bara hili kwa ujumla.
Maendeleo huletwa na watu wenyewe; hayawezi kuletwa kutoka juu, hata kama watawala wangekuwa na nia njema na dhamira yao ni kuwatumikia watu wao kwa dhati. Wananchi ndio wanaoumizwa na umasikini uliokithiri, na ye yote anayetaka kuwatumikia hana budi kuwasikiliza na kuyatia matakwa yao maanani.
Aidha, wananchi si vipofu; wana macho na wanaona kwamba hao hao watawala wao wanaowajengea ‘shule’ zisizokuwa na walimu na zahanati zisizokuwa na wauguzi wanao utaratibu mbadala wa kuwasomesha watoto wao na kuwapatia matibabu wanapougua.
Si muda mrefu uliopita mtawala mmoja katika mojawapo ya mikoa alikuwa kitetea ujenzi wa ‘shule’ hizo na kuwahimiza wananchi wapeleke watoto wao. Wananchi walikuwa wanamjua mkubwa huyo na walijua watoto wake wanasoma shule ya kweli, yenye walimu na vitabu na kila aina ya vifaa vya kufundishia, ikiwa ni pamoja na kompyuta.
Walipomuuliza ni kwa nini yeye hakupeleka watoto wake katika shule hizo, akawa mkali kweli kweli na mjadala ukaishia hapo.
Napenda kufunga sehemu hii ya makala hizi kwa kusisitiza kwamba iwapo tunataka kujenga mustakabali unaoeleweka kwa ajili ya Taifa letu hatuna budi kujenga utaratibu unaoeleweka wa kutoa huduma muhimu za msingi kwa watu wote wa nchi hii, na huduma hizo ni elimu na afya.
Tujenge shule za kweli kwa kufundisha walimu na kuwapa nyenzo za kufundishia. Tujenge zahanati za kweli kwa kufundisha wauguzi wa kutosha wa ngazi ya msingi watakaosambaa katika vijiji vyetu ambako ndiko wanakoishi watu wetu walio wengi na ndiko waliko wazalishaji wa chakula kinachotuweka hai.
Bila shaka watakuwapo Watanzania wachache watakaotaka kuwapa watoto wao elimu tofauti (nchini au ughaibuni), au watakaotaka kuwapeleka Afrika Kusini kila wanapopata mafua, wafanye hivyo kwa utashi wao wa anasa, lakini nchi iridhike kwamba watoto walio wengi wanapata elimu ya daraja la kwanza na matibabu maridhawa bila kulazimika kuuza nyumba zao au ng’ombe wao.
Siku tutakapofikia hatua hiyo, bila shaka tutakuwa tumeachana na malumbano yasiyoisha hivi sasa baina ya Serikali na wanafunzi wa vyuo vikuu kuhusu ‘uchangiaji’ wa gharama za elimu, mivutano ambayo mimi naiona kama isiyokuwa na maana kwa sababu uwezo wa kuwasomesha vijana hawa tunao. Tunachotakiwa kufanya ni kuutambua ulipo na kuupeleka hadi kwenye tatizo.
Niliandika mapema kwamba mara nyingi tumeambiwa kwamba tunapenda kukosoa matendo ya watawala bila kutoa mapendekezo ya njia mbadala. Nimejaribu kutoa mapendekezo yangu, na bila shaka wako wengine wengi wenye mapendekezo kama yangu, na yaliyo tofauti. Basi tuyajadili. 

No comments:

Post a Comment