Dk. Slaa hekima imepita kiti cha enzi
Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 15 December 2010
Kisima cha Mjadala
MOJA ya makala niliyoandika mara baada ya uchaguzi mkuu, ilihusu
kiongozi mmoja wa kale ambaye dini zote kubwa za Uyahudi, Uislamu na
Ukristu zinamtambua kutokana na uongozi wake wa hekima.
Mfalme
Solomoni (Sulemani) ambaye maandiko yanatudokeza kuwa alikuwa na hekima
kubwa katika uongozi, licha ya matatizo katika maisha yake binafsi.
Aliitwa mtu mwenye hekima kupita wote waliowahi kuishi.
Ninafahamu watu wengi wanataka “viongozi wasomi” wengine wanataka “viongozi vijana” na wengine wanataka “viongozi bora.”
Wapo wanaotaka vyote vitatu. Sijasikia wanaptaka viongozi wenye hekima.
Tatizo la hekima ni kwamba haiji kwa kuvishwa shahada - iwe ya kusomea au heshima.
Hekima huja kwa mtu kujaliwa kipaji ambacho anakiendeleza kwa kutumia uzoefu na ujuzi.
Lakini kama jamii haina viongozi wenye hekima, basi jamii jamii hiyo ina matatizo.
Ninapoangalia mambo yaliyotokea katika chaguzi mbalimbali ambazo
zilizofanana na zile za kwetu kwenye utangazaji wa matokeo, ninajikuta
niwe wa kwanza kutoa shukrani kwa mtu ambaye nilimuunga mkono na
kumpigia debe kuwa rais, Dk. Willibrod Slaa.
Leo nimedhirika
kwamba nilikuwa sahihi. Dk. Slaa amethibitisha kuwa siyo Raila Odinga,
siyo Quattara na wala siyo Morgan Tsvangarai.
Hawa watatu na
mwenzao wa kule Haiti walifikia mahali pa kuweka rehani maisha ya
mataifa yao ili waweze kupata nafasi ya kuingia madarakani.
Kabla ya hekima kutawala, Dk. Slaa alikuwa na haki ya kutaka matokeo ya
uchaguzi yasimamishwe na kwa hakika baada ya kukataa matokeo
yalivyotangazwa alikuwa na haki ya kiasili ya kuyapinga na kuwashawishi
wananchi kumuunga mkono.
Hata uamuzi wa kutotambua matokeo
yaliyompa rais Kikwete ushindi, aliuchukua kwa tahadhari kubwa ili
kuokoa taifa lake lisiingie katika machafuko.
Kwa maneno
mengine, Dk. Slaa angeweza kuonesha kiu ya madaraka na kulazimisha siasa
za kupata uongozi siyo kwa sanduku la kura tena bali kwa kuwasubiri
wasuluhishi, Thabo Mbeki na Koffi Annan.
Lakini baada ya
matokeo na hali tete iliyokuwepo nchini, Dk. Slaa aliamua kuchukua
mkondo mwingine. Hekima ilipiga hodi mlangoni kwake na kukihoji: “Ili
kiwe nini?”
Wapo walioandika na kusubiri kwa hamu wasikie Dk. Slaa aseme neno ambalo lingechochea mwamko wa mapambano.
Baadhi ya vijana walikuwa wanasubiri kwa hamu tu kusikia neno la kwenda
mitaani kudai haki yao. Hilo lingefanyika, sote kama taifa tungejikuta
katika matatizo makubwa ya kisiasa.
Yangekuwa ni matatizo
ambayo yangeweza kweli kusababisha “mazungumzo ya muafaka” kufanyika na
hatimaye kwa namna moja au nyingine, Dk. Slaa “kuingizwa madarakani.”
Ni njia iliyotumika Zanzibar na sasa tunamuona Maalim Seif Sharrif
Hamad akikatiwa saluti na vyombo vya dola kama makamu wa kwanza wa rais
wa visiwa hivyo.
Lakini mwitikio wa Dk. Slaa baada ya hali hii
tete umenithibitisha kwa asilimia mia moja kuwa linapokuja suala la
uongozi, yeye huwa anasimama peke yake.
Kama Watanzania
hawajafikiria kumshukuru na kumpa mkono wa asante, naona mimi
nimshukuru. Ninamshukuru kwa mambo kadhaa makubwa.
Kwanza,
ametuthibitishia kuwa hana kiu ya madaraka. Taifa hili linashuhudia
viongozi kutoka upinzani na kwenye chama tawala wakisema lolote na
kufanya chochote ili aidha, waingie madarakani au wabakie madarakani.
Wengine wanapovuliwa madaraka wanaona ni ugomvi na kuwaona wananchi kama ni maadui.
Wapo wengine ambao tunaambiwa baada ya kupoteza nafasi zao, wameamua
hata kutoendeleza miradi waliyokuwa wanaifadhili wakati walipokuwa
madarakani. Sababu, wamepoteza madaraka.
Dk. Slaa ameonesha
tofauti. Ni mwanasiasa mahiri na mwenye umakini. Ukiangalia maneno
yaliyokuwa yanatolewa wakati wa kampeni, mtu angeweza kuamini kuwa
angeweza kudai madaraka kwa nguvu.
Kwani ukweli ni kwamba amekubalika na zaidi ya watu milioni 2.2 (bila kujali uchakachuaji).
Pili, sina budi kusema asante kwake kwa sababu ametuonesha kitu ambacho
ni nadra kufanywa na wanasiasa wengi. Hufikiri kabla ya kusema.
Kati ya mambo ambayo ninaamini wanasiasa wetu vijana wa pande zote
mbili wanahitaji kujifunza, ni ile tunu ya ukimya na kutokuharakisha
kuzungumza au kutenda.
Kuna wakati kiongozi unatakiwa utulie na
kusikiliza pande zote, upime uzito wa unachosikia ili hatimaye uweze
kutumia hekima kufanya uamuzi sahihi.
Ninafahamu mara baada ya
uchaguzi na matokeo kuanza kuonekana kuvurugwa, Slaa alipokea ujumbe wa
tofauti na kutoka makundi mbalimbali.
Wapo waliotaka aongoze
maandamano ya kupinga Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), na wapo waliotaka
ajitangaze mshindi (kama ilivyotokea huko Ivory Coast ambako sasa kuna
watu wawili wanajiita marais).
Nina uhakika wapo wengine
waliotaka wapate nafasi ya kutolea usongo mafisadi. Wapo viongozi
mbalimbali wa kidiplomasia na kidini waliojaribu kwa ushawishi wote
kumtuliza Dk. Slaa ili “kudumisha amani na utulivu.”
Kitendo cha kuwa kimya na kuwasikiliza kimetupa mwanga kuwa yeye si mtu wa kukurupuka katika maamuzi.
Tatu, baada ya matukio ya “kulinda kura” kwenye majimbo mbalimbali
nilikuwa na hofu sana na kuandika kitu cha kuwataka vijana watulie kwa
sababu siyo mwisho wa dunia.
Kulikuwa na watu wengi waliojawa hasira na wengine walioona kuwa wamedhulumiwa haki yao.
Tatizo ni kuwa kuna watu ambao wanafikiri vijana wanaelewa sana hili la “umoja na utulivu.”
Ushahidi umekuwa wazi kabisa (kama ulikuwa unaangalia TV wakati ule)
kuwa vijana wanaanza kuchoka. Dk. Slaa aliweza kutulia na kutofanya kitu
ambacho kingechochea hisia za vijana. Sote tunajua nini kingetokea.
Nani ambaye hakuona kilichotokea London wiki iliyopita ambapo mwana wa
Mfalme, Charles na mke wake Camilla walishambuliwa na waandamanaji?
Ninachosema ni kuwa wapo watu watakaopongezana na wapo ambao watapeana tuzo na sifa mbalimbali za ushindi.
Wenyewe wataona wanastahili heshima wanayopewa. Lakini ukiniuliza mimi
nimekolewa na nini, nitakuambia kuwa nimekolewa si kwa matendo haya,
bali kwa maamuzi ya Dk. Slaa.
Nina uhakika hakuna taasisi
nchini yenye ujasiri wa kusema wazi “asante Dk. Slaa.” Hakuna chuo
ambacho kinaweza kutoa tuzo ya wazi kwa Dk. Slaa kwa kumpa heshima
ambayo amejistahilisha.
Naamini wapo watu wengi tu ambao japo
wanafahamu ukweli wa kilichotokea, hawana ujasiri wa kumpigia simu au
kukaa naye na kumsikiliza. Hivyo ndivyo ilivyo.
Lakini
ninaamini, wale ambao wanataka kuwa wa kweli katika dhamira zao, wanajua
kabisa kuwa taifa hili limenusurika kuwa Haiti, Kenya, Ivory Coast au
Zimbabwe, si kwa matendo ya walio madarakani, bali kwa hekima ya Slaa.
Hivyo basi, hata kama CHADEMA imeamua kumtambua rasmi Dk. Jakaya Mrisho
Kikwete kuwa rais, sote tujue kabisa yamewezekana hayo kwa sababu ya
Slaa.
Hata kama hatuwezi kumtunukia nishani yoyote lakini tunaweza kusema asante.
No comments:
Post a Comment