Uislam wa CCM na Ukiristo wa CHADEMA
Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 06 April 2011
Tafakuri
NALAZIMIKA kuandika makala hii ili kutoa mchango wangu juu ya mjadala
tete unaoendelezwa na viongozi wa dini na wanasiasa. Kwa kuwa imekuwa
kawaida kwa watu kuzungumzia suala hili jumlajumla tu.
Nalazimika kusema wazi kuwa makala hii imechochewa na matamshi na nasaha
za Shehe Mkuu, Mufti Simba kwa waislam kwa nyakati tofauti hivi
karibuni.
Mambo mawili katika mengi aliyoyatamka ni lile la
kuwataka waislam wasihudhurie mikutano na maandamano ya chama cha
CHADEMA kwa kudai yanavunja amani. Pili, ni lile la kuwa Rais Jakaya
Kikwete anaandamwa na migogoro mbalimbali kwa sababu ya dini yake.
Nachelea kusema kuwa matamshi haya ni mazito kwanza, kwa sababu
yametamkwa na mtu mzito katika taifa letu, na pili, yanawagawa
Watanzania pasipo shaka.
Vyama vya siasa kama Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na CHADEMA ni taasisi za kibinadamu zenye nafasi finyu
isiyotosha kummiliki Mwenyezi Mungu ndani yake.
Kwa hiyo, madai
ya Mufti Simba ni mazito sana; kuwaambia watu wa dini fulani
wasifungamane na chama fulani kwa sababu tu chama hicho kinaonekana
kutofuata mafundisho na itikadi ya dini fulani.
Mungu ni mkubwa
na chama ni kitu kidogo sana, kwa hiyo sidhani kama itakuja kuwezekana
kumlazimisha Mungu aenee ndani ya chama fulani. Kimsingi ni jambo
lisilowezekana kuwalazimisha watu kukipenda chama fulani kama ilivyo
vigumu kuwalazimisha kuchukia chama fulani.
Hata pale CHADEMA
wanapoandamana na kudai wanaishitaki serikali kwa wananchi au pale
serikali inapotumia nguvu kuzuia CHADEMA isiichonganishe serikali na
wananchi, ni dhana za kufikirika kuliko uhalisia.
Mwenendo wa
serikali kupitia viongozi wake ndicho chanzo kikuu cha chuki waliyonayo
wananchi dhidi ya serikali. Kwa hili, CHADEMA isijipe umaarufu wa moja
kwa moja, na wala CCM na serikali yake wasiichangie CHADEMA kupata
umaarufu usio wake.
Ndani ya CCM kuna watu wa dini zote kama
ilivyo ndani ya CHADEMA. Uongozi wa vyama hivyo kuonekana kwa wakati huu
kuwa na viongozi wengi wa dini fulani, ni suala la muda lisiloweza
kumfanya kiongozi wa dini alazimike kuwaamuru waumini wa dini yake
kukikataa chama fulani.
Kwa kuwa ni suala la muda, upo
uwezekano wa uongozi huo kubadilika na kuweka viongozi ambao mufti
anawapenda na hapo mufti atapata taabu kuibadili kauli yake.
Mathalani, hivi sasa kiongozi mkuu wa CCM ni Muislam na mufti anaona
hiyo ni bora na kudiriki hata kusema anaandamwa kwa sababu ya dini yake.
Kiongozi mkuu wa CHADEMA ni Mkiristo, na mufti anawaamuru waislam
wasimfuate anapoitisha maandamano. Itakuwaje pale CCM itakapopata
kiongozi mkiristo na CHADEMA ikapata mwislamu?
Baadhi ya wenye
hekima wamehoji ni lini uislam umekuwa rafiki wa chama tawala kwa sababu
yako maandiko yaliyoibuka miaka ya karibuni yanayoonyesha kuwa dhuluma
kubwa imefanywa kwa waislam tangu tupate uhuru.
Ikiwa dai hili
ni kweli, iweje leo chama tawala kilindwe na waislam kwa kukitetea
kisiteswe na maandamano ya “maadui wa amani na mshikamano” wa taifa
letu? Najiunga na wanaohoji kwa sababu, naamini kabisa kuwa uislam na
ukiristo ni zaidi ya mtu mmoja aliye kiongozi katika taasisi.
Tukijenga hoja zetu na misimamo kwa sababu ya mtu aliye madarakani
katika chama fulani, tutajinyima thawabu tunayoitafuta kwa udi na uvumba
katika dini zetu.
Nikirudi katika madai ya mufti kuwa Rais
Kikwete anaandamwa kwa sababu ya dini yake, nitaje mshtuko wangu juu ya
tamko hili. Macho yetu yameshuhudia wakristo na viongozi wao wakimuunga
mkono Rais Kikwete.
Mchungaji Lusekelo (Mzee wa Upako) amelipia
kipindi maalum cha kuwaonya Watanzania ili waache kumnyooshea kidole
Rais Jakaya Kikwete maana adhabu ya kufanya hivyo yaweza kuwa ni
“kukatwa shingo.”
Wachungaji Getrude Lwakatare na Temba
wamefanya kampeni na maombezi nchi nzima kumuunga mkono Rais Kikwete.
Maaskofu kadhaa kutoka Anglikana na KKKT wamegombea ubunge kupitia CCM
kwa kuvutiwa na uongozi wa Kikwete kwa CCM na hata kutumia mtaji wa
kukubalika kwao japo kwa bahati mbaya haikutokea.
Wako wabunge
waislam wameshinda katika majimbo yenye wakiristo wengi na hata Kikwete
mwenyewe kujizolea kura nyingi katika mikoa yenye wakiristo wengi
akimwacha mbali mgombea mkiristo. Hii yote inadhihirisha kuwa Rais
Kikwete anaungwa mkono na wakristo.
Naweza kusema pasipo shaka
kuwa uislam wa aina ya matamshi ya mufti ndio unaweza kutia kasoro
mapenzi waliyonayo wakristo kwa Rais Kikwete. Tamko la namna hii
linawakatisha tamaa wale wasio wa dini ya Rais Kikwete.
Kwa
ushauri tu, ikiwa kweli mufti anaona Rais Kikwete anaandamwa, amtazame
Rais Kikwete kama rais na siyo kama mwislamu. Mabadiliko haya ya mtizamo
yanaweza kuibua ukweli uliofichika kuwa, kati ya wanaomwandama wamo
wakristo na waislam na wanafanya hivyo kama wajibu wao kwa Rais
waliyemchagua kwa hiari yao.
Ni hatari kumlinda rais kwa silaha
bandia ya udini usiokuwapo, hali inayoweza kumfanya (kama haijamfanya!)
Rais kulazimika kutazama matatizo ya nchi kwa kutumia miwani ya udini
na hata kujaribu kuyatatua kwa kutumia udini. Matatizo ya taifa letu ni
makubwa kuliko udini wa kulazimisha au kuchonganisha vyama na wanachama
wake.
Wala matatizo ya taifa letu hayawezi kutatuliwa na amani
ya bandia inayohubiriwa na baadhi ya viongozi wa dini wanaojificha ndani
ya kauli mbiu hiyo ili kulinda ufisadi wa fikra zinazowatesa Watanzania
bila kujali dini zao.
Kwa jitihada hizi za kuisilimisha CCM au
kuibatiza CHADEMA, tunalichimbia kaburi taifa letu. Ifike mahali Rais
Kikwete ajitetee mwenyewe ili kukomesha tabia hii ya viongozi wa dini
kama mufti, Lusekelo, Temba na mama Lwakatare wanaojituma (kama
hakuwatuma) kuligawa taifa kwa kutumia itikadi za dini na siasa.
No comments:
Post a Comment