Kilichotokea Mbagala ni hasira za Waislamu? II
Evarist ChahaliUskochiToleo la 265
24 Oct 2012
KABLA ya kuingia kwa undani katika makala hii ambayo ni mwendelezo wa
makala iliyochapishwa katika toleo la wiki iliyopita, naomba niwasimulie
wasomaji mkasa ambao unaweza kuwa “funga kazi” katika utitiri wa
vimbwanga vya watawala wetu.
Wiki iliyopita, Naibu Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, aliwatia aibu Watanzania
akiwa Afrika Kusini alipodai kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inaundwa kwa Muungano kati ya kisiwa cha Bahari ya Hindi cha Pemba na
Zimbabwe. Ukidhani ninamsingizia, basi angalia video hii kupitia
kiunganishi hiki; http://goo.gl/uW6H2
Na licha ya kufanya madudu hayo, Mulugo ‘alilikoroga’ zaidi alipodai kuwa Muungano huo wa ‘Zimbabwe na Pemba’
ulitokea mwaka, (namnukuu) “one nineteen sixty-four.” Mwaka huo hauleti
maana yoyote, iwe kwa Kiingereza au kwa Kiswahili, kwani 1-19-64
inaweza tu kuleta maana kwa mfumo wa tarehe wa Marekani (yaani tarehe 19
mwezi wa kwanza mwaka 64).
Ninaomba nitamke bayana kuwa Naibu
Waziri Mulugo ni mzembe wa hali ya juu. Yawezekana aliandaliwa hotuba
hiyo, lakini haihitaji busara japo kidogo kuwa huwezi kukurupuka kutoa
hotuba kabla hujaipitia. Sijui Rais Jakaya Kikwete alijisikiaje baada ya
kuona video hiyo yenye hotuba ya Mulugo, lakini kwa kosa hilo la ajabu
kabisa, Naibu Waziri Mulugo sio tu anapaswa kutuomba radhi Watanzania
kwa kupotosha historia ya taifa letu bali pia ingefaa aondolewe katika
wadhifa wake unaoshughulikia elimu (elimu gani hiyo ambayo wakati
Tanzania ‘haijamalizana’ na Malawi kuhusu mpaka kwenye Ziwa Nyasa, yeye
‘anaihamasisha Zimbabwe ‘idai Pemba ni sehemu ya nchi hiyo?’)
Nisiongelee sana suala hilo bali ninawaachiwa Watanzania wenzangu kuhitimisha wenyewe kuhusu madudu haya ‘ya karne.’
Kama nilivyoahidi katika toleo lililopita, wiki hii ninaendelea na
mjadala kuhusu vurugu za kidini ambazo kwa siku za karibuni zinaonekana
kushika kasi.
Katika makala iliyopita, nilijaribu kuonyesha
sababu zilizojenga msingi wa manung’uniko ya Waislamu katika masuala ya
elimu na ajira. Mwishoni mwa makala hiyo niliuliza maswali yafuatayo
(ninajinukuu)
“Je; kilichotokea Mbagala ni hasira tu za baadhi
ya Waislamu waliochukizwa na kitendo cha ‘mtoto wa Kikristo’ kukojolea
Kuran Tukufu?
Je; udini ni tatizo kubwa katika Tanzania yetu
ingawa halizingumzwi vya kutosha? Binafsi, ninaamini jibu la swali hilo,
ni ndiyo. Kama ni ndiyo, kwa nini tunalikwepa tatizo hili?
Je; yawezekana udini ni turufu muhimu kwa baadhi ya wanasiasa mufilisi?”
Kwa swali la kwanza, nilishabainisha kwenye makala hiyo kuwa kwa
mtizamo wangu, vurugu hizo za Mbagala zilisababishwa na zaidi ya hasira
za baadhi ya Waislamu waliokasirishwa na kitendo cha mtoto kuikojolea
Kuran Tukufu.
Yayumkinika kusema kuwa hasira za baadhi (na
pengine ni wengi) ya Waislamu huko nyumbani (Tanzania) ni dhidi ya kile
kinachotajwa kama ‘Mfumo Kristo.’ Kwa kifupi, wanaoamini hivyo wanauona
mfumo huo unawapendelea Wakristo sambamba na kuwabagua Waislamu, hususan
katika sekta za elimu na ajira, ambazo kimsingi zinahusiana kwa karibu.
Japo, kama nilivyobainisha katika makala yangu iliyopita kuwa Ukristo
kwa kushirikiana na ukoloni ulichangia kutengeneza hali ya kutokuwa na
usawa katika elimu na ajira, haimaanishi moja kwa moja kuwa Wakristo
wanawabagua Waislamu. Naomba nieleweke hapa: kuna tofauti kati ya mfumo
na watu wanaonufaika au kuathiriwa na mfumo huo.
Ninasema hivyo
kwa sababu, wakati hoja ya kuwa Wakristo wanawabagua Waislamu ingeweza
kuwa na mashiko wakati wa utawala wa Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na Awamu ya Tatu ya Rais
Benjamin Mkapa, ambao wote ni Wakristo, ni vigumu kwa hoja hiyo kuwa na
uzito kwenye Awamu ya Pili na hii ya sasa (ya Nne) za marais Waislamu
Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete.
Hata hivyo, kwa mtizamo
wangu, viongozi hao wote wanne, hawawezi kukwepa lawama kuwa kwa kiasi
kikubwa hawajafanikiwa sio tu kuyatupia macho kwa makini malalamiko ya
Waislamu bali pia wamekuwa wakikwepa kuyashughulikia kwa uzito
unaostahili.
Angalau kwa upande wa Baba wa Taifa tunaweza
kukubaliana kuwa sio tu kwamba alishakiri kuwa kukosekana kwa usawa
katika elimu na ajira kwa Waislamu ni tatizo, lakini pia alikwenda mbali
zaidi na kujaribu kuukarabati mfumo wa elimu ili uweze kutoa fursa kwa
Watanzania wote bila kujali imani zao.
Ni muhimu kukumbuka kuwa
licha ya ukweli kuwa Mwalimu alikuwa Mkristo na mshika dini, mafanikio
yake katika harakati za kupigania uhuru yalichangiwa zaidi na Waislamu.
Lawama ‘kubwa’ inayoweza kuelekezwa kwa Mwalimu ni jinsi serikali yake
ilivyoshughulikia suala ‘nyeti’ la uundwaji Baraza la Waislamu Tanzania
(BAKWATA) na kupigwa marufuku Jumuiya ya Ustawi wa Waislamu wa Afrika
Mashariki (East African Muslim Welfare Society- EAMWS).
Kwa
kifupi, tangu kuundwa kwake, kwa kiasi kikubwa BAKWATA imeshindwa
kujitenganisha na serikali, na pia imeshindwa kufuta hisia kuwa ‘ni
chombo kinachotumiwa na serikali kuwagawanya na kuwakandamiza Waislamu.’
Japo EAMWS ilikuwa taasisi ya kidini lakini ilionekana kama ‘mkombozi
wa Waislamu’ hususan kwenye sekta ya elimu, na yayumkinika kusema kuwa
laiti kuundwa kwa BAKWATA kungeibua taasisi yenye ufanisi kama EAMWS,
basi pengine pengo lililopo kwenye maeneo ya elimu na ajira kati ya
Waislamu na Wakristo lingekuwa limepungua kwa kiasi kikubwa.
Ufinyu wa nafasi unaninyima fursa ya kuingia kwa undani kujadili hoja za
kuifungia EAMWS na hatimaye kuanzisha BAKWATA, lakini ukweli kwamba
serikali hiyo hiyo iliyoipiga marufuku EAMWS ilishiriki kikamilifu
katika uundwaji wa BAKWATA umechangia kudumu kwa hisia kuwa ‘BAKWATA
iliundwa kama chombo cha serikali dhidi ya Waislamu.’
Na katika
utafiti wangu, matokeo ya awali yanaonyesha Waislamu wengi
hawaridhishwi na mwenendo wa BAKWATA katika kutetea maslahi yao.
Kimsingi, moja ya jambo lilionekana ‘kuwaunganisha’ wahojiwa wangu wa
Kiislamu (ambao nilieleza katika makala iliyopita kuwa niliwagawanya
katika makundi mawili ya ‘walio na msimamo mkali’ na ‘wa kawaida’- kwa
minajili ya kiutafiti- ni suala hilo la BAKWATA.
Sasa katika
mazingira haya ambacho chombo pekee kikuu kinachotarajiwa kuwaunganisha
Waislamu kinaonekana kuwa kinawakandamiza, na-kuwanukuu baadhi ya
wahojiwa- ni sehemu ya ‘Mfumo Kristo’ ni wazi kuwa baadhi (na pengine
wengi) ya Waislamu wanajiona kama ‘mateka wa mfumo,’ kwa maana ya hisia
za kubaguliwa na Wakristo na kubaguliwa na chombo kinachopaswa kutetea
maslahi yao (BAKWATA).
Kwa mtizamo wangu, kuwa ‘mateka wa mfumo
usiokubalika’ kunasababisha kuuchukia, na kama tujuavyo, chuki huzaa
hasira. Hasira hizo zinasubiri mazingira ‘mwafaka’ ili zichomoze
hadharani. Na tukio kama la Mbagala lilitoa ‘fursa mwafaka’ kwa hasira
hizo.
Na ‘hasira’ hizo zinatoa jibu la swali la pili kuhusu
udini. Kwamba Waislamu wanawachukia Wakristo, sitaki kuamini hivyo.
Kwamba Waislamu (baadhi au wengi) wanachukizwa na mfumo wanauona kuwa
unawabagua na kuwapendelea Wakristo, binafsi jibu langu ni ndio.
Na kwa vile ni vigumu kutofautisha ‘Mfumo Kristo’ na Wakristo kama
waumini wa dini, ni muhimu kutambua kuwa kwa namna fulani-kubwa au
ndogo- kuna uhasama wa kisaikolojia au kihisia kati ya madhehebu haya
mawili. Kinachosaidia ‘kuficha’ uhasama huo ni misingi iliyojengwa huko
nyuma ambayo ilisisitiza zaidi Utanzania wetu kuliko Uislamu au Ukristo
wetu.
Kwa bahati mbaya-au makusudi-misingi hiyo inavunjwa kwa
nguvu na wanasiasa waliokuja baada ya Mwalimu Nyerere. Kwa kifupi,
wakati siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ilijenga misingi ya kutuunganisha
Watanzania tuwe kitu kimoja, ‘ubabaishaji’ uliofuatwa-kwa mfano
kinachoitwa Azimio la Zanzibar- umechangia sana kukuza ombwe
lililotokana na ‘kifo cha Ujamaa,’ na wakati huo huo kutoa fursa kwa
wenye ‘hasira’ zao kuziweka hadharani.
Kama nilivyowahi
kuandika katika makala moja huko nyuma kuhusu unafiki wetu kuhusu suala
la ushoga (hoja kubwa ikiwa ni imani zetu za kidini na mila na desturi
zetu), kuna unafiki unaoendelea katika sio tu kuzungumzia suala la udini
kwa uwazi zaidi bali pia hakuna utashi wa kisiasa (na hata kijamii)
kukabili tatizo hili.
Ni nani asiyejua kuwa wakati wa utawala
wa Mwinyi kulikuwa na baadhi ya Wakristo waliokuwa wakinung’unika chini
chini kuwa teuzi za Mwinyi zilikuwa zinapendelea Waislamu? Ni nani pia
asiyejua kuwa alipokuja Mkapa lawama kama hizo ziliendelea kuwapo chini
chini kuwa Mkapa alikuwa akiwapendelea Wakristo? Na ni nani
atakayejifanya hajui kuwa utawala wa Rais Kikwete umekuwa ukilaumiwa
chini chini kuwa unawapendelea Waislamu?
Ninafahamu kuna
watakaosema hizi ni hisia zangu tu. Hawa ndio ninaowaita wanafiki. Na
unafiki huu ndio miongoni mwa vikwazo vikubwa vya kujadili tatizo la
udini, na vurugu zinazohusishwa na tatizo hilo, kwa hofu ya kuitwa
mdini. Niseme hivi, bora niitwe mdini kwa kujitoa mhanga kuanzisha
mjadala wa suala hili kuliko ‘nionekane mwema’ ilhali tunalipeleka taifa
letu mahali kusikofaa.
Nitajitahidi kuhitimisha mfululizo wa
makala hizi kuhusu vurugu za kidini kwenye toleo lijalo, au pengine
makala mbili zijazo. Hata hivyo, nihitimishe makala hii kwa jibu fupi
kwa swali la tatu kuhusu udini unavyotumiwa na wanasiasa mufilisi kwa
minajili yao binafsi.
Ninaamini sote tunakumbuka jinsi kampeni
za uchaguzi mkuu uliopita zilivyogubikwa na tuhuma za udini. Na hapa
nisiume maneno: chama tawala CCM kilifanya kila jitihada kuufanya
‘upadri’ wa mgombea wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, kuwa turufu muhimu
ya kumnyima kura za Waislamu. Hili nitalijadili kwa kirefu katika makala
ijayo, lakini kwa namna fulani, CCM haiwezi kukwepa lawama kuwa ni
miongoni mwa vyanzo vya vurugu za kidini tunazoshuhudia hivi sasa.
Chama cha siasa kinapoamua kwa makusudi kuwagawa wapiga kura kwa
misingi ya imani zao za kidini, kinaandaa ‘viungo’ kwa ajili ya vurugu
za kidini. Na ikumbukwe kuwa ni CCM hii hii iliyowahadaa Waislamu kuhusu
kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi (huku ikitambua kuwa haina dhamira ya
dhati ya utekelezaji wa ahadi hiyo) na hadi sasa inaendelea kucheza
danadana katika suala hilo.
Nimalizie makala hii kwa
kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa tuna kila kitu cha kupoteza
(everything to lose) kwa kutengana kwa misingi ya kidini na hatuna cha
kupoteza (nothing to lose) tukiendelea kuwa wamoja, kama majeruhi wa
ufisadi, umasikini, magonjwa na dhahma nyingine zinazotukabili ambazo
hazijali imani zetu za kidini. Ili Tanzania yetu ifike mahala
tunapotamani ifike, au inapostahili kuwa, ni lazima tuwe kitu kimoja.
Tukumbuke, UMOJA NI NGUVU NA UTENGANO NI UDHAIFU
No comments:
Post a Comment