Freemasons ni ‘abrakadabra’
Maggid MjengwaToleo la 244 RAIA MWEMA
20 Jun 2012
TUNAWAPITISHA watu wetu kwenye njia yenye giza. Kwenye njia yenye matope. Kwanini?
Kwenye moja ya mashairi ya Marcelino Dos Santos wa Msumbiji anasema; "
We Must Plant". Kwa maana ya tuna lazima ya kupanda. Dos Santos
hazungumzii kupanda mbegu za mahindi au mtama, bali kupanda fikra za
kimapinduzi kwa wanajamii. Fikra zitakazowasaidia kutoka katika hali
iliyopo na kwenda kwenye hali nyingine iliyo bora zaidi.
Na
Socrates, mwanafalsafa wa Uyunani ya kale alipata kuonekana akimulika
kurunzi mchana wa jua kali. Inaandikwa, kuwa Socrates yule alizunguka
sokoni na kurunzi (tochi) yenye kumulika. Watu walimwuliza, kulikoni?
Socrates akawajibu; ”Kwenye nuru hii , kuna walio gizani.”
Kwa
Socrates lilikuwa ni tendo la kifalsafa lenye kuelezea hali halisi. Hata
katika dunia hii ya kisasa, bado tuna miongoni mwetu, walio gizani
mchana wa jua kali. Angalia ya kwa ’ Babu’ wa Loliondo. Ndiyo, kuna
wanaohitaji kumulikiwa mwanga.
Uvumi wa Freemasons unaosambaa
sasa kwenye jamii ni dhana ya kufikirika kama ilivyokuwa kwa Babu wa
Loliondo. Ya Babu wa Loliondo yalianza kwa uvumi wa magazetini na
hatimaye kugeuka kuwa moja ya majanga ya kitaifa.
Leo
Watanzania tunajua, kuwa pamoja na kutangazwa sana, Babu wa Loliondo
hajamtibu hata mgonjwa mmoja. Badala yake, amechangia kwenye vifo na
mateso ya wengi. Hakika, ni sisi Watanzania ndio tuliokuwa ' wagonjwa'
wa kuendekeza abracadabra za Babu wa Loliondo.
Na uvumi huu wa
sasa wa Freemasons ni abrakadabra nyingine tunayolishwa Watanzania. Ni
habari za kupotosha jamii, ikiwamo jamii kuaminishwa kuwa wanachama wa
jumuiya ya Freemasons ni watu matajiri na kuwa anayejiunga na Freemasons
atapata utajiri wa haraka.
Kwamba Freemasons inahusishwa pia
na nguvu za giza ikiwamo imani za kimashetani. Walioanzisha upotoshaji
huu wanajua kuwa hiyo Freemasons ni jumuiya ya kimataifa kama ilivyo kwa
Rottery na Lions Club ambazo uanachama wake haupo wazi kwa yeyote yule
bila kupitia wanachama wenyewe. Lakini haimaanishi kuwa wanachama wa
jumuiya hizo wanajipatia utajiri wa haraka kwa kushiriki ‘ abrakadabra’ .
Leo hii hapa Tanzania kuna vijana wanaoshinda vijiweni wakiwaza tu
namna ya kujiunga na Freemasons badala ya kufanya kazi. Na Freemasons
pia imekuwa njia ya baadhi ya wanajamii kutetea uvivu wao. Freemasons
inatumika pia kuwaandama wenye kufanya kazi kwa bidii na kujipatia
mafanikio. Maana, leo hata anayenunua pikipiki mpya ataitwa ‘
Freemason!’
Ni wakati sasa kwa Serikali kutoa tamko juu ya hili
la uvumi wa Freemasons. Iweke wazi kuwa jambo hili linakuzwa na kuwa
kuna upotoshaji unaofanywa kwa makusudi. Maana, uvumi huu ukiachwa
uendelee unaweza kutuletea madhara makubwa huko twendako.
Tunajua, kuwa leo wamejitokeza matapeli wanaowahadaa wanajamii kuwa wao
ni Freemasons na kuwa wanaweza kuwasaidia wengine kujiunga na mtandao
huo. Wamejitokeza pia waganga wa kienyeji wenye kufanya utapeli kwa
kutangaza kuwa wana uwezo wa ‘ kiganga’ wa kuwasaidia wateja wao
kujiunga na Freemasons. Wapo wanajamii wanaopoteza fedha na mali zao
kwa kutapeliwa juu ya hili la Freemasons. Ndiyo maana, kuwa ni wajibu wa
Serikali kuingilia kati kuwanusuru watu wake.
Ndiyo, watu wetu
wako kwenye giza. Kuna upumbavu unaendelea kwenye jamii. Ni wajibu wa
Serikali yao kuwasaidia kwa kuwamulikia mwanga. Na kuna tofauti ya
ujinga na upumbavu. Marehemu Mzee Jongo alipata kutamka;” Kusoma si
kuufuta ujinga, bali ni kuupunguza”.
Kila mwanadamu ana ujinga
wa jambo moja au mia moja. Kuwa na ujinga wa jambo si kosa, hata profesa
anaweza asijue namna ya kuchochea kuni za kuchomea mhindi mbichi.
Kijana wa darasa la saba anaweza kuwa hodari wa jambo hilo kumshinda
profesa.
Lakini upumbavu ni ile hali ya mwanadamu kufanya jambo
isivyotakiwa huku akiwa na uelewa wa namna ya kufanya inavyotakiwa. Huo
ndio upumbavu. Na ndiyo maana binadamu kuitwa mpumbavu ni tusi. Kuitwa
mjinga si tusi, kila mmoja ana ujinga wake. Kuwa na ujinga wa jambo
fulani ni kutoelewa jambo hilo. Ni nani anayeelewa kila jambo?
Na mwanadamu unafanyaje unapoamka na kukuta dunia unayoishi ardhi yake
imeanza kumegeka na kuchotwa na bahari? Kuna niliyemwuliza swali hilo.
Naye akanijibu; ” Huo ndio utakuwa mwisho wa dunia!” Aliyenijibu alikuwa
amechoka kufikiri. Nilidhani amgetamka, kuwa angeanza kujifunza
kuogelea. Maana, kwa kuogelea majini angeweza kukutana na kisiwa, au
nchi kavu.
Wanadamu tumejaliwa akili ili tuweze kufikiri. Na
kufikiri ndiko njia mojawapo ya kuiteka kweli. Kufikiri kunahamisha
milima na hata kuiweka kando kuruhusu mwanga upite. Inakuwaje basi
mwanadamu anapoacha kufikiri? Haya ya ya kuendekeza abrakadabra za
Freemasons ni kielelezo cha Watanzania, kama ilivyokuwa kwa Babu wa
Loliondo, kuamua kuacha kufikiri. Ndiyo, kuna waliojifunika vilemba vya
ujinga. Wako gizani, wanahitaji mwanga.
Kuna wakati Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, aliingilia kati na kusitisha abrakadabra ya DECI
iliyokuwa ikiitafuna jamii. Pinda aliwanusuru wengi. Ni wakati sasa kwa
Waziri Mkuu wetu Pinda kuingilia tena kati na kulitolea tamko hili la
abrakadabra ya Freemasons. Kufanya hivyo atawanusuru wengi.
No comments:
Post a Comment