Wednesday, October 31, 2012

Suluhu ya uongo wa Malawi na ukimya wa Tanzania



Rai Mwema Toleo la 265
24 Oct 2012
HIVI karibuni yameibuka tena malumbano kuhusu mpaka baina ya Tanzania na Malawi. Malumbano haya ni mwendelezo wa fikra za aliyekuwa Rais wa Malawi, Kamuzu Banda kwamba, Malawi inayo miliki ya eneo lote la Ziwa Nyasa kulingana na makubaliano ya Wajerumani na Waingereza ya mwaka 1890.

Hata hivyo baada ya kulitafakari suala hili na kupata misimamo tofauti, sasa ni bayana kuwa Malawi haikuwahi kupewa wala kujitangazia umiliki wa eneo lote la Ziwa Nyasa.

Ajabu kubwa zaidi ni kwamba pia Malawi haikujadiliwa wala kuandikwa katika makubaliano ya Heligoland. Hivyo inashangaza ni jinsi gani Malawi imeweza kujiingiza kinyemela katika wahusika wa makubaliano yale na kuisukuma Tanzania katika kupambana na uhalali wa makubaliano badala ya upotofu wa tafsiri ya Kamuzu Banda.

Mshangao huu unazidi kukua inapoonekana kuwa Malawi inaanza kufanikiwa katika kuishinikiza Ujerumani iyakane majukumu, matakwa na maumivu yake kuhusiana na makubaliano yale.

Zipo sababu tatu zinazonifanya niamini kuwa Malawi au Rhodesia ya wakati ule si mhusika katika makubaliano ya Heligoland na pia makubaliano yale si ufumbuzi wa mgogoro baina ya Malawi na Tanzania.

Sababu ya kwanza ni kwamba majadiliano ya Heligoland hayakuhusu himaya ya Malawi, Rhodesia au eneo la kusini magharibi la “German East Africa”. Pili, makubaliano yale hayakuhusu umiliki wa eneo lolote la mto, ziwa au bahari. Kadhalika, makubaliano yale hayakuhusu mipaka baina ya himaya au nchi tofauti.

Kuhusu dhana ya kuchangia mipaka, ramani za miaka ya 1890, na hadi miaka ya 1930, zilionyesha mipaka miwili iliyoenda sambamba, ambayo iliachana kabisa kuelekea kingo tofauti za mito au maziwa makubwa. Kwa maana hii himaya iliyoitwa Rhodesia ilikuwa na mpaka wake katika ukingo wa magharibi wa Ziwa Nyasa, sambamba na ule wa “German East Africa” uliokuwa ukingo wa mashariki mwa ziwa hilo. Kwa utaratibu huo Ziwa Nyasa lilibaki katikati ya himaya hizo za kikoloni kama eneo lisilokuwa na ardhi au jamii ya kutawaliwa kama koloni.

Kwa vile Ziwa Nyasa halikumilikishwa mwaka 1890, Wajerumani na Waingereza waliligombea mwaka 1914, ambapo Ujerumani ilishindwa na kuondolewa katika eneo lote la Tanganyika. Baada ya hapo, Uingereza ilikuwa na uhuru na uwezo wa kuamua lolote kuhusu umiliki wa Ziwa Nyasa.

Hata hivyo, nyaraka zilizopo zinaonyesha kuwa hakuna uamuzi wowote uliofanyika kuhusu jambo hilo. Historia inaonyesha kuwa baada ya uhuru, Rais Nyerere alifanya mawasiliano akitaka kujadiliana na Serikari ya Malawi kuhusu umiliki wa ziwa hilo, ambapo Rais Kamuzu Banda alijibu kwamba makubaliano ya Heligoland yanaweka bayana mpaka wa Malawi na Tanzania ni kingo za Ziwa Malawi.

Banda alisema: "But our terms are clear on this. According to the 1890 Heligoland agreement between Britain and Germany, the border between Malawi and Tanzania is the edge of the waters of Lake Malawi.

Kifungu cha makubaliano ya Heligoland ambacho Rais Banda alikipotosha na kukitumia kinyemela ni kile kinachoainisha mwisho wa ardhi ya “German East Africa”, upande wa kusini magharibi, ambacho kilisomeka kwamba: “To the south by the line that starts on the coast of the northern border of Mozambique Province and follows the course of the Ruvuma River to the point where the Messinge flows into the Ruvuma. From here the line runs westward on the parallel of latitude to the shore of Lake Nyasa. Turning north, it continues along the eastern, northern, and western shores of the lake until it reaches the northern bank of the mouth of the Songwe.”

Tafsiri ya kifungu hicho ninayoipata mimi ni kwamba hakikuwa sehemu ya makubaliano au makabidhiano. Badala yake kifungu hicho ni sehemu ya utambuzi wa ardhi ya Tanganyika au “German East Africa”, ambayo haikuwa na uhusiano au mgusano na ardhi ya Rhodesia au Malawi. Japokuwa kifungu hicho kimeandikwa katika makubaliano hayo, hakikutokana na makubaliano ya kukabidhiana vipande vya ardhi vilivyohusika.

Badala yake kifungu kile ni sehemu ya maelezo kuhusu upana wa ardhi ya “German East Africa”. Hakuna sehemu yoyote ya makubaliano yale inayotaja ukaribu au ujirani na himaya nyingine ng’ambo ya maji kama vile Malawi, (Rhodesia) Zambia, Kenya, Burundi, DRC, Uganda, India, Msumbiji au Australia.

Kwa vile Ziwa Nyasa halikuwahi kugawanywa au kumilikishwa, watawala wa Kiingereza waliokuwa upande wa Malawi waliendelea kukiri, kukariri na kukazia kila mwaka ukweli kuwa hawakuwa na miliki ya eneo lote la ziwa hilo.

Nimejitahidi kutafuta mwaka ambapo walikiri hivyo kwa uwazi ulio mkubwa zaidi, na nimegundua kuwa pengine ni mwaka wa 1936, ambapo ripoti ya serikali yao ilikuwa na kifungu cha maneno kilichosema kuwa: “The Nyasaland Protectorate consists of a strip of land some 520 miles in length and varying from 50 to 100 miles in width, bounded on the east by Lake Nyasa, on the south by Portuguese East Africa, on the west by North-Eastern Rhodesia and on the north by the Tanganyika Territory”.

Ingekuwa bora zaidi kama viongozi wa Tanzania wangethibitisha haraka ubatili na upotofu wa mawazo ya Rais Banda. Badala yake Serikali ya Tanzania iliamua kuachana naye kwa matumaini kuwa ingetokea nafasi ya kujadiliana na viongozi wenye busara au bashasha zaidi baada ya utawala wake.

Ni kweli kuwa viongozi hao tayari wametokea na kushika madaraka huko Malawi, ambapo Rais wa sasa ni Joyce Banda. Pamoja na mabadiliko hayo ya kiutawala, bado ni vigumu sana kuziona busara za Banda huyu iwapo Tanzania haitafanikiwa kuibatilisha na kuibomoa kabisa tafsiri potofu iliyojengwa na Banda wa kwanza.

Badala ya kuonyesha upotofu wa tafsiri iliyopandikizwa na Kamuzu Banda, Tanzania imejikita zaidi katika kupingana na makubaliano ya Heligoland, na kusisitiza kwamba raia wake wanaoishi jirani na Ziwa Nyasa wanazo haki za msingi za kuteka maji ya kunywa na kuvua samaki. Japokuwa hatua kama hizo ni muhimu sana, ukweli ni kwamba haki hizo za Mwenyezi Mungu hazitokani na huruma ya Malawi, wala utetezi wa Tanzania, au hata hukumu ya mamlaka yoyote duniani.

Yapo mambo mawili yanayoweza kubatilisha au kuharibu haki za kuteka maji na kuvua samaki kwa upande wa Tanzania. Jambo la kwanza ni uwezekano wa kuimilikisha Malawi jamii za wakazi wa Mbeya, Njombe na Songea, kama Rais Banda alivyowahi kudai na kuona haraka kuwa haingewezekana kabisa.

Jambo la pili, ambalo linawezekana na linaelekea kabisa, ni kujengeka kwa huruma, utetezi au hukumu kuelekea kuiachia Malawi itekeleze mipango ya uharibifu endelevu wa rasilimali za maji, samaki, na viumbe asilia ndani ya Ziwa Nyasa.

Kwa vile ni dhahiri kuwa Malawi haiwezi kuzuia Watanzania kupata haki za kuchota maji, kuvua samaki na kufanya shughuli za kiasili katika Ziwa Nyasa, ni bora Serikali ya Tanzania iwe makini ili kuepuka uwezekano wa kupuuzwa au kuliwazwa kwa kupewa haki hizo.

Jambo la msingi ni kwamba serikali za Malawi na Tanzania zinawajibika kujenga matumizi endelevu ya rasilimali katika Ziwa Nyasa. Katika kufanya hivyo serikali hizi zinawajibika kukubaliana na kuutangazia ulimwengu ni kwa kiwango gani zimefanikiwa kushirikiana katika kutekeleza matakwa ya kimataifa, ambayo ni kuwajibika katika shughuli za maendeleo kwa ushirikiano, badala ya kugawana au kugombea maji.

Bila kuainisha maeneo ya ushirikiano wa pamoja, na bila kupigana vita, mamlaka za kimataifa haziwezi kuona umuhimu wa kutoa hukumu inayohusu mgawanyo wa maji ya Ziwa Nyasa.

Jambo pekee linaloweza kupatikana ni kupuuzwa na kuambiwa kuwa “Nendeni kwanza mkazungumze na kushirikiana katika kutekeleza mipango endelevu ambayo nyote mnalazimika kuikubali”.

Baadhi ya mambo hayo ni kuzuia uvuvi haramu, kulinda mazingira, kusaka majambazi, na kufanya utafiti. Iwapo Serikali ya Tanzania inajihusisha na mikakati kama hiyo ni rahisi kuonyesha kuwa inahitaji matumizi ya boti za doria, askari wa majini na silaha za moto. Kwa maana hii ni muhimu Tanzania iweke bayana majukumu ya msingi inayohitaji kutekeleza ndani ya Ziwa Nyasa yanayohusu maendeleo ya watu wa kawaida, na ni kwa kiasi gani baadhi yake yanakwazwa au kuchafuliwa na shughuli zinazoendelea upande wa Malawi.

Shughuli mojawapo ambayo inatajwa sana ni matarajio ya Malawi kutaka kuchimba mafuta ndani ya ziwa. Bila kujali mafuta yanayotafutwa na Malawi yapo upande wa kusini, magharibi au mashariki, Serikali ya Tanzania inao wajibu wa kuweka pingamizi na kuzuia harakati hizo zisiendelee bila kuwapo mikataba miwili mahsusi ya Ziwa Nyasa.

Mkataba wa kwanza ni ule utakaohusu matumizi endelevu ya maji safi na uhai wa viumbe na mkataba wa pili ni ule wa kuzuia au kudhibiti uchimbaji wa mafuta ndani ya ziwa. Mikataba ambayo Tanzania inataka kutumia katika mzozo huu inaeleza wazi kuhusu usafi wa maji na uhai wa viumbe asilia, bila kujali mipaka ya kisiasa au ile ya kikoloni.

Ziwa Nyasa ni hazina ya maji safi na viumbe adimu duniani, ambavyo kwa ujumla wake vina thamani kubwa zaidi kuliko mafuta au hata dhahabu. Ni makosa kabisa kufikiri kwamba mafuta ni bora kuliko maji safi na viumbe hai ndani ya ziwa.

No comments:

Post a Comment