Ndimi mbili za Zitto na kisa cha mkata kuti alilokalia
Evarist Chahal
10 Oct 2012
MIONGONI mwa faida ninazopata kutokana na uandishi wa makala katika
jarida hili maridhawa, ni mawasiliano ya kila wiki na baadhi ya
Watanzania wenzangu. Wengi wa ninaowasiliana nao, ni wasomaji ambao kwa
namna moja au nyingine huwa wameguswa na mada ninazoongelea. Kuguswa
huko hufuatiwa na ama pongezi au kukosolewa. Wakati mara nyingi pongezi
huandamana na maneno ambayo si tu yananipa moyo na ujasiri zaidi wa
kuendelea na uandishi wa makala hizi, mara nyingi kukosolewa huambatana
na maneno yasiyopendeza kuyasoma au kuyasikia popote pale.
Baadhi ya wanaopongeza safu hii hudiriki kwenda mbali zaidi na kushauri
labda nifikirie kuingia kwenye siasa. Mara zote jibu langu huwa lile
lile. Najisikia fahari kuwatumikia Watanzania wenzangu kupitia uandishi
wa makala, huku nikiamini kuwa si lazima kuwa mwanasiasa ili uweze
kutekeleza jukumu hilo ipasavyo.
Lakini kwa upande mwingine,
baadhi ya wanaonikosoa huenda mbali zaidi na kunituhumu kuwa uandishi
wangu umeelemea kwenye chuki binafsi, husda na vitu kama hivyo. Jamaa
mmoja alifikia hatua ya kudai kuwa makala zangu ni sehemu tu ya mikakati
wa dini yangu dhidi ya utawala unaoongozwa na mtu anayetoka dini
tofauti na yangu.
Kama ambavyo ninaridhishwa na pongezi kuhusu
safu hii, huwa ninajifunza jambo moja au jingine kutoka kwa wakosoaji
wangu (wengi wao hupenda kuhifadhi majina yao halisi). Kukosolewa huko,
kunanisaidia kwa kiasi fulani, na hasa tukizingatia ukweli kwamba ukiona
unamwagiwa sifa tu pasipo kuelezwa japo kasoro kidogo, basi yayumkinika
kuhisi kuwa kuna mushkeli mahala fulani.
Nimelazimika kuandika
hayo kutokana na ukweli kwamba makala yangu katika toleo lililopita
ambayo pamoja na mambo mengine ilimzungumzia mbunge wa Kigoma Kaskazini
kupitia CHADEMA, Zitto Zuberi Kabwe, imetafsiriwa na baadhi ya wasomaji
wangu kama sehemu ya kampeni zangu za kumkwamisha kuingia ‘Ikulu.’
Nimeshaeleza mara kadhaa katika baadhi ya makala zangu zilizopita kuwa
mimi si mwanachama wa chama chochote kile cha siasa, na nimekuwa hivyo
kwa miaka kadhaa, tangu nikiwa huko nyumbani. Wakati, kwa kiasi kikubwa
nilipokuwa huko nyumbani sheria ilikuwa inanikataza kuwa mwanachama wa
chama chochote cha siasa, kwa sasa uamuzi wangu wa kuwa neutral
unachangiwa zaidi na imani yangu kuwa itikadi bora zaidi kwa mwananchi
ni uzalendo na kuitumikia jamii kwa hali na mali.
Moja ya sifa
kuu za sheria, ni kwamba iwe mbaya au nzuri, inabaki kuwa sheria hadi
itakaporekebishwa au kuondolewa. Kuna nyakati tunalazimika kufuata
sheria zinazokinzana na haki zetu (kimsingi sheria inapaswa kuendana na
uwiano kati ya haki na wajibu), lakini tunalazimika kuzifuata kwa vile
ndizo sheria zinazotawala.
Ni kwa mantiki hiyo, ninarejea tena
kutofautiana na Zitto katika dhamira yake ya kutaka kuwa Rais wa
Tanzania, kwa sababu kwa mujibu wa sheria tulizonazo, hatokuwa na sifa
ya urais hapo mwaka 2015 kutokana na kuwa na umri pungufu ya ule
unaotajwa kwenye sheria mama ya nchi, yaani Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Ninaafikiana na Zitto kwamba sheria hii ni ya
kionevu kwa sababu kama inawezekana kwa mtu wa miaka 40 kuwa Rais
kwanini ishindikane kwa mtu mwenye miaka 39?
Hata hivyo,
napenda kumfahamisha kuwa hadi hapo sheria hiyo itakaporekebishwa au
kubadilishwa, pamoja na ‘ubaguzi’ inaoubeba, itaendelea kuwa sheria
inayopaswa kufuatwa. Na kwa vile kwa mazingira ya kawaida tu inatarajiwa
Rais kuwa miongoni mwa vinara wa si tu kufuata sheria, bali pia
kuzilinda, itakuwa ni ‘utani mbaya’ kwa mtu anayetaka kuwa Rais
kudhamiria kuvunja sheria kama hiyo inayokataza walio chini ya miaka 40
kugombea urais.
Nimesema ninamuunga mkono Zitto kwamba sheria
hiyo ni ya kibaguzi. Lakini kama tunachukia ubaguzi kwenye sheria, basi
pia tunapaswa kuchukia ubaguzi kwenye kila eneo, iwe kwenye jinsia,
imani, asili, rangi na hata kundi la mtu katika jamii. Siku chache
zilizopita, kulikuwa na taarifa za kwamba Zitto aliongea na kituo kimoja
cha redio jijini Dar es Salaam na kutamka maneno yafuatayo:
“Wazee wetu walitusaidia sana kutupatia maendeleo ya kisiasa, sasa ni
jukumu letu kuleta maendeleo ya kiuchumi. Ila naomba nisisitize kuwa
jukumu hilo haliwezi kutekelezwa na mtu yeyote aliyezaliwa kabla ya
uhuru, na ninatangaza nitagombea urais mwaka 2015.”
Binafsi,
ninahitimisha kuwa kauli hiyo ni ya ubaguzi wa mchana kweupe. Lakini
pia, licha ya ubaguzi, inaonekana kichekesho kwani imetoka kwa
mwanasiasa (Zitto) ambaye hajawahi kuficha hisia zake dhidi ya ubaguzi
wa watu kwa vigezo vya umri. Tukiweka kando taratibu za ndani ya CHADEMA
kupata mgombea wake, moja ya sababu kuu zinazoonekana kama kikwazo kwa
dhamira ya Zitto kuwa Rais, ni hiyo tuliyoiongelea hapo juu ya
kutotimiza umri wa miaka 40 mwaka 2015 kama inavyotajwa kwenye Katiba.
Tunaomsapoti Zitto katika hoja yake hiyo, tunazingatia ukweli kwamba
japo nchi haiwezi kuongozwa na mtoto wa miaka mitano, kwa mfano, mtu
yeyote mzima (kiumri) anaweza kuiongoza nchi yetu pasipo umri wake
kuathiri utendaji kazi wake. Utu-uzima si umri maalumu bali masafa
(range) ya umri. Utu-uzima unaendana zaidi na uwezo wa mtu kutambua
wajibu wake na kumudu kuutekeleza.
Wajibu huo unaweza kuwa
katika ngazi ya familia (kama vile kuoa/kuolewa) au katika jamii pana,
kama vile kushika dhamana ya uongozi.
Kwa hiyo, kimsingi, kama
Zitto amemudu kuwatumikia wapigakura wa jimbo la Kigoma Kaskazini kwa
mihula miwili sasa, sambamba na kulitumikia taifa kupitia uenyekiti wake
kwenye Kamati ya Bunge, basi hakuna sababu ya msingi kwa umri wake kuwa
kigezo cha kumzuwia kugombea urais mwaka 2015 hata kama atakuwa
hajatimiza miaka 40. Ndiyo. Katiba inazuwia, lakini ukweli ni kuwa
inazuwia kiuonevu!
Sasa wakati tunaafikiana na Zitto kupingana
na uonevu huo wa Katiba, inakuwaje tena anatumia kigezo cha umri
kuwabagua ‘wazee’ anaodai hawawezi kutuletea maendeleo ya kiuchumi?
Busara ndogo tu ingeweza kumfahamisha Zitto-kama msomi-kuwa siasa na
uchumi ni maeneo yanayotegemeana. Kama wazee waliozaliwa kabla ya Uhuru
walimudu kutuletea maendeleo ya kisiasa, kwanini washindwe kwenye
maendeleo ya kiuchumi?
Kama yeye aliyezaliwa baada ya Uhuru
ameweza kufanya kazi nzuri kabisa katika uongozi wake wab kisiasa, ni
kigezo kipi anachotumia kuwaona wazee waliozaliwa kabla ya Uhuru kuwa
hawatoweza harakati za kuleta maendeleo yetu? Kwa hakika kabisa, huu ni
ubaguzi, na kamwe mtu mwenye hisia za ubaguzi hapaswi japo kufikiriwa
kuongoza nchi yetu.
Ninasema hivyo kwa sababu kama alivyotuusia
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ubaguzi huzaa ubaguzi. Leo
itakuwa “wazee waaliozaliwa kabla ya Uhuru hawawezi kutuletea maendeleo
ya kiuchumi,” kesho itakuwa “Wakristo/Waislamu hawawezi kufanya hili,”
“Wapogoro hawawezi kufanya lile,” au “wanawake hawawezi jukumu Fulani na
kadhalika.
Naomba nimpe darasa dogo tu Mheshimiwa Zitto kuhusu
kikwazo halisi cha maendeleo yetu. Uhaba unaozidi kukua katika uzalendo
wa Mtanzania. Uzalendo hauna umri. Historia inatufundisha mengi tu
kuhusu mchango wa wazee katika maendeleo ya sehemu zao husika. Mwalimu
Nyerere, Nelson Mandela, Mahatma Ghandhi na kadhalika.
Binafsi,
niliwahi kupishana kimtizamo na Zitto kwenye mtandao wa kijamii wa
Twitter, ambapo katika hali ya kuchokoza mjadala, nilitamka kuwa muundo
wa Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba haukuzingatia uwiano kati ya
Wakristo na Waislam. Zitto alikerwa sana na hoja yangu hiyo aliyoiita ya
kibaguzi. Alisisitiza kuwa tunapaswa kuangalia wasifu wa wajumbe kwa
kigezo cha uwezo na uzoefu wao na si imani zao za kidini.
Cha
kushangaza, ndani ya miezi michache tu, mtu huyo huyo aliyekemea vikali
virusi vya ubaguzi (wa dini), amegeuka mfuasi wa ubaguzi wa umri. Kama
tunapojadili teuzi mbalimbali tunapaswa kuangalia uwezo na uzoefu wa
mteuliwa, kwanini basi wazee waliozaliwa kabla ya Uhuru wasitizamwe kwa
uwezo na uzoefu wao kutuletea maendeleo ya kiuchumi, badala ya
kuwahukumu kwa umri wao?
Ninaibua changamoto kama hiyo ya
‘ubaguzi’ kwa minajili, si ya kukwaza dhamira ya Zitto kuingia Ikulu
mwaka 2015, bali kumsaidia kuamsha tafakuri yake iwapo utekelezaji wa
dhamira hiyo utakuwa na manufaa kwake na kwa chama chake, au utaishia
kuwa njia ya mkato kwa CCM kurejea madarakani huku CHADEMA ikiishia
kuonekana chama cha mapambano kati ya vijana na wazee kukimbilia Ikulu.
Nimalizie makala haya kwa kukumbushia tena kauli ya Baba wa Taifa, ya
kwamba yatupasa kuwaogopa kama ukoma wale wote wanaokimbilia Ikulu. Kama
sisi wengine tunaweza kuitumikia nchi yetu kupitia makala zetu, huku
wanasiasa kama Zitto wakimudu kututumikia kama wabunge, kisa cha
kukimbilia Ikulu ambako Mwalimu alituasa kuwa anayefanya hivyo aogopwe
kama ukoma, ni cha nini?
Simshawishi Zitto aachane na ndoto
zake za urais kwani ninatambua hiyo ni haki yake ya kidemokrasia. Hata
hivyo, ni muhimu kwa mwanasiasa huyo kijana kutambua kuwa wapenda
mabadiliko ya kweli watamwona kama msaliti pindi ndoto zake hizo
zitakapoishia kuwa kikwazo kwa CHADEMA kuing’oa CCM madarakani. Japo
busara zinatueleza kuwa na ndoto pekee haitoshi, bali ni muhimu
kutekeleza ndoto hizo kwa vitendo, ukiota unakata kuti unalokalia, na
ukiamka ukaamua kulikata, sote tunajua matokeo yake.
No comments:
Post a Comment