Kilichotokea Mbagala ni hasira za Waislamu?
Raia MWEMA
Evarist ChahaliUskochiToleo la 263
17 Oct 2012
KWA mara nyingine, wiki iliyopita Tanzania imeshuhudia ‘sura mbaya’
(ugly face) ya imani ya kidini. Kwa mujibu wa taarifa zenyewe,
kilichoanza kama mchezo wa watoto kilisababisha vurugu kubwa
zilizopelekea makanisa zaidi ya matano kuchomwa moto, sambamba na
uharibifu wa mali kadhaa.
Inaelezwa kwamba chanzo cha vurugu
hizo ni kitendo cha mtoto mmoja kuikojolea Kuran Tukufu baada ya
‘mabishano ya kitoto’ na mtoto mwenzie. Habari zinasema mtoto aliyefanya
kitendo hicho alitaka kuthibitisha ukweli wa ‘tishio’ alilopewa na
mtoto mwenzie kuwa iwapo atakikojolea Kitabu hicho Kitukufu, basi
atageuka nyoka!
Sote tuliwahi kuwa watoto katika hatua za
mwanzo za maisha yetu, na kwa kutumia uzoefu huo kama ‘watoto wa zamani’
tunaweza kukumbuka vitu vya ajabu, vya kukera, vya kuchekesha, na vya
kila aina ambavyo twaweza kuvihitimisha kwa msemo huu wa Waingereza:
‘kids will always be kids’ (watoto wataendelea kuwa watoto).
Kwamba binadamu, pasipo kujali umri wake, anaweza kukojolea Kitabu
Kitukufu cha dini fulani, ni jambo lisilopendeza hata kidogo. Na kwa
hakika, kitendo cha aina hiyo, kitamchukiza kila muumini wa dini husika.
Lakini kama ilivyo katika maeneo mengine ya maisha ambapo umri
unaangaliwa kama kigezo muhimu cha kuhukumu tendo, ukweli kwamba
aliyekojolea Kuran Tukufu ni mtoto wa miaka 14, ulipaswa kupewa uzito na
baadhi ya waumini wa dini ya Kiislam ambao waliamua kuchukua sheria
mkononi kwa kufanya vurugu kubwa ikiwa ni pamoja na kuchoma moto
makanisa.
Licha ya kuguswa na tukio hilo la kusikitisha kama
Mtanzania na Mkristo, lakini pia nimeguswa kwa vile linahusiana na eneo
ambalo nimekuwa nikihangaika nalo kitaaluma kitambo sasa. Miaka michache
iliyopita, nilikuja huko nyumbani kukusanya data kwa ajili ya utafiti
wa kitaaluma kuhusu harakati za vikundi vya Kiislam nchini Tanzania. Kwa
sababu zilizo nje ya uwezo wangu, utafiti huo bado haujakamilika japo
katika hatua niliyofikia unaweza kutoa majibu fulani kuhusu
kinachoendelea huko nyumbani hivi sasa.
Nilipata fursa ya
kuzungumza na makundi makuu mawili ya waumini wa dini ya Kiislam. Wale
tunaoweza kuwaita ‘wenye msimamo mkali’ na wale wa ‘wenye msimamo wa
kawaida.’ Naomba nisisitize kuwa matumizi ya maneno ‘msimamo mkali’ na
‘kawaida’ ni kwa minajili ya mjadala tu. Ninatoa tahadhari hii mapema
kwa kuchelea uwezekano wa shutuma kuwa ninawagawa Waislam katika
makundi, ambayo kama ilivyothibitika katika utafiti wangu, wengi wao
hawapendi mgawanyo wa aina hiyo kwani wanaamini wote ni Waislam.
Moja ya mambo yaliyojitokeza katika mahojiano yangu na ‘makundi’ yote
mawili ni manung’uniko (grievances) ambayo yamedumu kwa muda mrefu.
Manung’uniko hayo yameshamiri zaidi kwenye suala la usawa katika elimu
na ajira. Wahojiwa wengi walionyesha kuwa na hisia ya kubaguliwa kati
yao na Wakristo katika upatikanaji wa fursa za elimu na ajira. Kimsingi,
ukimnyima mtu fursa ya elimu, unatengeneza mazingira ‘mazuri’ ya
kumkwaza kupata ajira.
Takwimu mbalimbali nilizokusanya katika
utafiti huo, zinaweza kusapoti madai hayo. Lakini la muhimu zaidi hapa
si sapoti ya takwimu hizo, bali mazingira yaliyopelekea uwepo wa hali
hiyo. Kutokana na ufinyu wa nafasi ninalazimika kutoa maelezo ya jumla
kwani kupitia kipengele kimoja hadi kingine kunahitaji zaidi ya makala
moja.
Kwa kifupi, moja ya sababu zilizopelekea ‘ubaguzi’ katika
upatikanaji wa fursa za elimu na ajira kati ya Waislamu na wasio
Waislam (hususan Wakristo) ni mfumo wa utawala wa kikoloni. Kama
tunavyofahamu, wakoloni walikuwa Wakristo, na tunafundishwa kwenye somo
la historia kuwa miongoni mwa ‘watangulizi wa ukoloni’ walikuwa
wamisionari wa Kikristo.
Moja ya mbinu zilizotumiwa na
wamisionari kutengeneza mazingira mazuri ya kutawala jamii za Kiafrika
ni ‘kusilimisha,’ japo neno hilo lina maana zaidi kwenye Uislam.
Ninalitumia hapa kwa maana ya kuwatoa watu kutoka katika imani yao ya
awali na kuwaingiza katika imani mpya.
Lakini historia
inatufundisha kuwa Uislam ulifika huko nyumbani karne kadhaa kabla ya
Ukristo. Kwa bahati mbaya au makusudi, walioleta Uislam walikuwa
wafanyabiashara kutoka Arabuni na Mashariki ya Mbali, na hawakuwekea
mkazo sana kusambaza dini yao.
Yayumkinika kuhitimisha kwamba
kushindwa kwa watangulizi hao wa Uislam kueneza dini hiyo miaka kadhaa
kabla ya ujio wa Wamisionari na hatimaye wakoloni, kulichangia
kurahisisha kusambaa kwa Ukristo kwa ama ‘kusilimisha’ Wapagani
(ninatumia neno hili kumaanisha dini za asili za Kiafrika) na Waislam.
Tukifupisha historia, mkoloni alitumia Ukristo kama moja ya njia za
kuzitawala jamii zetu. Ni katika mazingira hayo, stadi mbalimbali
zinaonyesha kuwa kwa namna fulani baadhi ya Wakristo walichelea kuunga
mkono mapambano dhidi ya mkoloni kudai uhuru wetu hasa kwa vile wakoloni
walifanikiwa kwa kiasi fulani kuulinganisha ukoloni na Ukristo (yaani
kumpinga mkoloni ni sawa na kumpinga Yesu/Mungu).
Kwa kutumia
Ukristo kama njia ya kurahisisha utawala wao, wakoloni pia walitumia
dini hiyo kama chombo cha kuwatenganisha watawaliwa. Kimsingi, kuna aina
ya mwafaka wa kitaaluma kuwa si kwamba wakoloni waliwathamini sana
Wakristo wa Kiafrika, bali waliwaona kama nguzo muhimu katika kuigawa
jamii, na hivyo kuwarahisishia kiutawala jamii husika.
Ingawa
kuna wamisionari waliokuja Afrika kwa minajili ya kidini halisi, wengi
wao waliendelea kushirikiana na utawala wa kikoloni katika maeneo
mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utoaji elimu. ‘Ushirika’ huu wa
wamisionari na wakoloni katika utoaji elimu, unaweza kuelezewa kama
mwanzo wa ujenzi wa tabaka la Wakristo wenye elimu na ‘wasio Wakristo’
(hususan Waislam) wasio na elimu.
Kadhalika, baadhi ya Waislam
walichelea kujiunga na taasisi za elimu za wamisionari/wakoloni kwa
kuhofia kuingizwa katika dini hiyo (Ukristo). Tukiweka hali ilivyokuwa
kabla ya uhuru, mazingira yaliyojitokeza baada ya kuondoka mkoloni,
yameendelea kwa kiasi fulani kurutubisha ‘ubaguzi’ huo wa elimu na
ajira.
Baada ya kupata uhuru, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere alikiri hadharani kuwa kuna umuhimu wa kurekebisha hali ya
kutokuwapo usawa wa kielimu kati ya Wakristo na Waislam. Licha ya
jitihada zake kubwa, hadi anaondoka madarakani ‘usawa’ huo haukuweza
kufikiwa kwa kiwango cha kuridhisha.
Kuna maelezo mengine hapa.
Shule za seminari za Wakristo ambazo kimsingi ni maalum kwa ajili ya
‘kuzalisha’ viongozi wa makanisa, zilikuwa ‘zikizalisha’ kundi la wasomi
wa Kikristo ambao kwa sababu moja au nyingine, hawakuishia kuwa
viongozi wa kanisa, bali wakachukua ajira serikalini au kwenye taasisi
nyingine. Kwa upande mwingine, shule za kidini za Waislam ziliegemea
zaidi kwenye utoaji elimu ya kidini, na katika mazingira hayo, tofauti
na ilivyo kwa seminari, ‘hazikuzalisha’ wasomi wa kutosha kuingia kwenye
ajira serikalini (naomba nieleweke kwa makini hapa).
Kwamba
utawala wa Mwalimu Nyerere uliwapendelea Wakristo na kuwabagua Waislam,
ni jambo ambalo halijathibitika kitaaluma. Hoja hiyo ni miongoni mwa
masuala yanayojenga manung’uniko kwa baadhi ya Waislam. Kwamba baadhi ya
Wakristo, hususan waliotoka seminari na kujiunga na ajira serikalini,
waliwabagua Waislam na kuwapendelea Wakristo, ni jambo ambalo
halijathibitika kitaaluma ingawa linawezekana kinadharia na kimantiki.
Kimsingi, tatizo si ubaguzi wa msomi/mwajiri Mkristo dhidi ya
mwanafunzi/msaka ajira Muislam, bali mfumo ambao ulijengeka wakati wa
ukoloni na umeendelea kuwepo. Unatoa nafasi (on merit) kwa Wakristo
zaidi ya Waislam. Kama mwajiri anataka kujaza nafasi kwenye ofisi yake,
anapaswa kuangalia, pamoja na mambo mengine, sifa za kitaaluma za waomba
kazi. Sasa kwa vile mfumo wa elimu tuliorithi kwa mkoloni, na kama
nilivyobainisha hapo juu, unatengeneza wasomi wengi wa Kikristo kuliko
wa Kiislam, ni dhahiri kutarajia ‘ubaguzi’ wa nafasi za ajira.
Majuzi tumefanya sensa. Watawala wetu wamegoma kujumuisha kipengele cha
dini kwa madai mbalimbali. Lakini kwa kufanya hivyo, watawala
wanajinyima fursa ya kuelewa, kwa mfano uwiano wa ajira kati ya Wakristo
na Waislam. Na cha muhimu hapo si kuelewa tu, bali pia kutafuta namna
ya kurekebisha hali hiyo. Na hili ni tatizo la msingi linalofanya
‘tatizo la dini’ kuendelea kuwapo. Kuna hisia kwamba kwa kujaribu
kulizungumzia suala hili kwa uwazi, kutazua tafrani kubwa kuliko
mwafaka. Lakini sote tunajua kuwa ugonjwa hautibiki kwa kujidanganya
kuwa haupo mwilini!
Je; kilichotokea Mbagala ni hasira tu za
baadhi ya Waislam waliochukizwa na kitendo cha ‘mtoto wa Kikristo’
kukojolea Kuran Tukufu? Binafsi, naamini kuna sababu za ndani zaidi ya
‘hasira’ hizo na zinazosababisha ‘hasira’ hizo. Je; udini ni tatizo
kubwa katika Tanzania yetu ingawa halizingumzwi vya kutosha? Binafsi,
ninaamini jibu la swali ilo, ni ndiyo. Kama ni ndiyo, kwanini
tunalikwepa tatizo hili?
Jibu linaweza kupatikana kwenye tatizo
jingine ‘lisilozungumzika’ la kero za Muungano wa ‘Tanganyika’ na
Zanzibar. Kwa kifupi, hadi sasa hakuna utashi wa kisiasa na kijamii
kulikabili tatizo hili. Kwenye Muungano, kila Rais anachelea kuvunjikiwa
na Muungano, ambao Baba wa Taifa ‘alishatoa radhi’ kwa atakayeuvunja.
Kwenye hili la udini, viongozi wetu wanakwepa kulikabili kwa kuchelea
kuonekana wadini. Kibaya, baadhi yao walitumia udini kwenye kampeni za
uchaguzi mkuu uliopita. Je; yawezekana udini ni turufu muhimu kwa baadhi
ya wanasiasa mufilisi?
No comments:
Post a Comment