Nani anasema kweli kuhusu Kigamboni?
26 Sep 2012 RAIA MWEMA
RAIS Jakaya Kikwete amekanusha kutouza ardhi ya Kigamboni kwa George
Bush. Sawa, lakini hajakanusha kuuzwa kwa eneo la Kigamboni. Kama
halijauzwa kwa Bush basi tuambiwe limeuzwa kwa nani.
Habari hii ya Kigamboni inarejesha suala la Richmond: nani alijua na nani alitaka kuchukua hatua kuzuia mkataba ule usiingiwe.
Leo tunapoambiwa habari ya Kigamboni mradi wa mji mpya uliojaa ubabe na usiri mkubwa tunapata tabu sana kuamini kauli hizi.
Mambo haya yanauma sana kwa wahanga wa zoezi hilo la mradi wa mji mpya
Kigamboni. Sisi Kigamboni tunajua tumeuzwa lakini pengine hatuna uhakika
tumeuzwa na nani na kwa nani. Mawakala wengi wanapitapita kurubuni
wananchi waukubali mradi, tena wengine ni viongozi.
Madiwani wa
Kata za Tungi, Vijibweni, Kigamboni-Ferry na Mjimwema wana mahusiano
mabaya sana na wananchi wao tangu siku ile walipoonekana kwenye runinga
bungeni Dodoma. Wanatuhumiwa kuendesha uwakala wa uuzaji wa Kigamboni.
Wapo wengine pia wakijinadi kama wawekezaji wa upanuzi wa bandari,
wajenzi wa kiwanda cha samaki, wawekezaji wa mafuta, kuna watoto wa
vigogo pia wanarandaranda huku wakitumia majina ya wazazi wao, nk.
Hatua ya kutimuliwa kwa Mbunge wa Kigamboni kwenye Bunge iliwafanya
wakazi wa Kigamboni kuamini kuna jambo linaendelea kuhusiana na suala
zima la utwaaji wa ardhi ya Kigamboni.
Wananchi hao wa
Kigamboni walimtuma Mbunge wao akaukatae mradi wa mji mpya wa Kigamboni
bungeni kutokana na kugubikwa na utata, usiri na ubabe. Kitendo cha
kumtimua Mheshimiwa Faustine Ndungulile bungeni kilionyesha juhudi za
kumshona mdomo na hivyo kuhalalisha dhuluma dhidi ya wakazi wa
Kigamboni.
Kama hiyo haitoshi, wakazi wa Kigamboni tuliandaa
mkutano mkubwa wa mapokezi ya Mbunge wetu pale uwanja maarufu wa
Machava. Walihudhuria wananchi kutoka Pembamnazi, Yaleyale Puna,
Kimbiji, Kibugumo, Mwongozo, Gezaulole, Chekeni Mwasonga, Tundwi
Songani, Mikwambe, Kibada, Kisarawe II, Mbagala yote hadi Mbande,
Chamazi na Mvuti.
Wanachi walikuwa wamechangishana mamilioni ya
shilingi kumkabidhi Mbunge huyo kama posho kufidia ile aliyonyimwa
kufuatia kutimuliwa bungeni na hivyo kumfanya kukosa posho za vikao. Cha
kushangaza sana na kwa masikitiko ya wana-Kigamboni, makaribisho hayo
yalisambaratishwa na jeshi la Kamanda Suleiman Kova saa chache kabla ya
makaribisho hayo kufanyika.
Lakini kwa mshangao mwingine, kuna
viongozi Kigamboni wanapitapita na kujitapa kwamba wao walihusika
“kulishawishi” Jeshi la Polisi kusambaratisha makaribisho hayo ya mbunge
kwa madai kwamba alikuwa anataka kuwachafulia hali ya hewa kwa
kuwahamasisha wananchi kuukataa mradi wa Mji Mpya Kigamboni.
Viongozi hao ni wale mawakala wa mradi ambao wametajwa hapo juu. Hivi
katika hali ya kawaida kiongozi wa kata au serikali ya mtaa anapata wapi
ujasiri na mamlaka ya kuamrisha Kanda Maalumu bila kuwa na msimamizi
huko juu? Hii haiwezi kuingia na kutulia tuli kwenye akili inayofanya
kazi maridhawa, vinginevyo itakuwa ni bongolala.
Wakazi wa
Kigamboni tumepewa katazo (stop order) la kutoendeleza maeneo yetu tangu
Oktoba 2008 kwa hoja kwamba ni eneo la mradi. Ilisemekana kuwa ramani
za satellite zilishachukuliwa kubaini kuna nini, wapi, na kwa nani.
Ukweli ni kwamba hakuna mkazi wa Kigamboni aliyeshirikishwa katika
zoezi hilo. Na nikiri tu hapa, kwamba hata hicho kilichomo kwenye hiyo
ramani hakuna anayejua. Mungu ni mkubwa akatuongoza vema, ramani hiyo
maarufu kwa jina la “Kigamboni: The Blue Diamond” ikaonekana kwenye
mitandao ya huko kwa George Bush. Ni fafanuzi (documentary) moja
inayofanyiwa maelezo (commentary) na mtu mwenye lafudhi ya Kimarekani
akisifia kuwa Kigamboni ni lango/kitovu (hub) ya “maendeleo” ya
Tanzania. Siwezi kuamini kwamba mwelezaji (commentator) yule ni Mmatengo
au Mhaya, na wala si Mndengereko au Mzaramu. Wasamaria wakatuvuta
masikio tukaiona hiyo documentary mtandaoni.
Nikueleze tu ndugu
msomaji kulikuwa na mwitiko (rush) mkubwa wa kuipata hiyo documentary
miongoni mwa sisi wadau wa Kigamboni. Tulikuwa tunanunua hiyo fafanuzi
ili kupata taarifa ambayo ni haki yetu kupata lakini wahusika serikalini
wakawa wanatuficha. Hata mimi binafsi niliuziwa na msamaria mwema Dar
es Salaam na ikawa bidhaa adimu hapa Dodoma.
Hayo ndiyo mazingira yaliyosababisha kujitokeza maneno (uvumi?) kwamba Kigamboni imeuzwa kwa George Bush.
Kwa mshangao wa tulio wengi, mara baada ya nusanusa yao serikalini
kugundua kwamba suala hilo liko hadharani kwa haraka sana Wizara ya
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikatoa kilichoitwa TAMKO LA SERIKALI
kwenye gazeti la Mwananchi Jumapili moja ya mwaka 2008 lililokataza
uendelezaji wa ardhi katika maeneo ya mradi kwa mujibu wa sheria ya
Mipango Miji namba 8 ya mwaka 2007. Katazo hilo lilitakiwa liishie
Septemba 2010 ambapo mradi ungekuwa umeanza awamu ya kwanza.
Hadi leo niandikapo makala haya hakuna kinachoendelea ukiachia mbali
kuwarudisha nyuma wakazi wa Kigamboni. Tumerudishwa nyuma kwani
tunatishwa (intimidated) kwamba chochote tutakachoendeleza kinakula
upande wetu. Choo kikianguka usikarabati maana itakula kwako. Na huo
wimbo wa fidia kwa mali za watu wa Kigamboni ni nyimbo za kila
mwanasiasa asiye makini. Nakumbuka mwanasiasa mmoja aliliambia Bunge la
Bajeti kwamba waathirika wa daraja la Kigamboni wameshathaminiwa mali
zao hivyo bado malipo tu. Mimi ni mmoja ambaye napitiwa na barabara ya
hilo daraja, lakini hadi leo niandikapo makala haya sijathaminiwa
kilicho changu.
Halafu anakuja mtu anasema watu wa Kigamboni
wamechochewa na wapinzani kupinga ujenzi wa daraja. Nachukia kauli za
aina hiyo maana ni za kudhalilishana.
Hivi Kigamboni kuna
ma-tabula rasa (wajinga) wanaosubiri wajuaji kutoka upinzani au chama
tawala kuja kuwaelekeza cha kufanya? Wote wenye fikra za aina hiyo
wanajidanganya na kama walizoea kunadi sera za aina hiyo sehemu
nyingine, Kigamboni wameula wa chuya. Wamuulize yule “mwekezaji” wa
kiwanda cha samaki pale Vijibweni mwaka 2004 akisaidiwa na kupigiwa debe
na aliyekuwa mkuu wa mkoa wakati huo aliishia wapi.
Tulikomaa
pale hatukutoka hadi leo tunapitiwa na barabara, nao wakituletea gozi
gozi, wembe ni uleule uliomnyoa “mwekezaji” wa kiwanda cha samaki.
Huwezi kusimama bungeni unadanganya umma umethaminisha mali za wananchi
pale Vijibweni wakati si kweli, halafu mtu anatarajiwa achekewe chekewe
tu. Mtu wa aina hii lazima aitwe kwa jina lake (call a spade a spade)
yaani kama ni mwongo basi aitwe hivyo bila kuumauma maneno.
Kama hakuna malipo hakuna barabara kupita pale Vijibweni na wala
hatuhitaji mwanasiasa wa upinzani au chama dola kuja kutusemea. Sisi
wahanga wa mradi huo tunajua kujisemea wenyewe. Tangu lini funza anikae
mimi halafu wewe ndiye uonyeshe wapi funza aliko mwilini mwangu? Hizo ni
falsafa zenye mtindio wa mwelekeo.
Badala ya kulaumu
wapinzani, Serikali ifanye wajibu wake kuhusu utata wa mji mpya
Kigamboni kwa kuwashirkisha wananchi katika hatua zote kama
alivyopendekeza Mbunge Ndungulile na kuungwa mkono na wana-Kigamboni.
Kule Kigamboni wakazi wameunda kamati yao ya kufuatitlia maendeleo ya
mchakato mzima wa mradi mji mpya. Wameshaongea sana kwenye mikutano ya
hadhara, wameongea na waziri, naibu waziri, katibu mkuu na watendaji
wengine serikalini na hata NGOs.
Mara nyingi viongozi wa kamati
wametokea kwenye runinga mbalimbali. Wafuatiliaji wa vipindi hivi
watakumbuka kwamba kamati ilihitimisha kwamba mradi wa Kigamboni ni EPA,
Richmond, Dowans, Deep Green, Tangold na miradi mingine ya kifisadi.
Mpaka leo hakuna aliyekanusha na kujenga hoja ya uhalali wa mradi huo.
Halafu si mara moja maofisa kutoka wizarani wameshatimuliwa na wananchi
kule Kigamboni lakini hakuna aliyesimama kuwatetea. Mambo (beacons)
zilizowekwa na mkandarasi bila wananchi kushirikishwa zimeshang’olewa na
wananchi, mbona hawachukuliwa hatua za kisheria kama beacons zile
ziliwekwa kihalali?
Kamati imeshatafiti na kugundua kuwapo
uvunjaji mkubwa wa sheria za nchi kwa upande wa Serikali katika
kutekeleza mradi huo. Hakuna aliyesimama kule serikalini na kutetea
utawala wa sheria unavyotumika katika kutekeleza mradi wa mji mpya kule
Kigamboni. Ni katika mazingira hayo mbunge wa Kigamboni Faustin
Ndungulile alisimama pale bungeni kutoa tamko la wakazi wa Kigamboni
kwamba mradi uanze upya kwa kufuata sheria ambazo Bunge limetunga.
Akaishia kutimuliwa bungeni kwa sababu ya kutetea haki za watu wa
Kigamboni lakini pia kutetea hadhi ya Bunge lenyewe.
Lakini
mheshimiwa huyo ni Mbunge wa chama dola si wa upinzani. Kwa mantiki hii
hoja ya kusema wapinzani wanapinga mradi wa mji mpya Kigamboni naiona ni
dhaifu sana na haina mashiko. Ukweli ni kwamba wananchi wa Kigamboni
kwa utashi wetu bila kusukumwa na chama chochote ndio tunaopinga mradi
huo unaoendeshwa kinyemela.
Hoja ya kuendeleza Kigamboni kwa
faida ya wananchi ni dhaifu na haina mashiko. Kama ukifanikiwa kuziona
zile picha (model impessions) za jinsi mji utakavyokuwa nadiriki kusema
hapa ni mji ambao wananchi wa Kigamboni hawamo katika makadirio yake.
Kule kuna eneo la viwanda, kuna eneo la utalii na burudani, kuna eneo la
biashara za kimataifa, kuna eneo la shule na vyuo vya kimataifa na eneo
la makazi ni asilimia kama 7% tu hivi. Wengine wamelibatiza eneo hilo
la makazi kuwa ni concentration camps.
Majengo yake ni
maghorofa yanayofikia 20 hadi 100. Mitaa yake hakuna njia za guta wala
mikokoteni. Bustani zake ni za maua si bamia, matembele, viazi wala
embe. Nyumba zake si za kupikia kwa kuni wala mkaa, hamna mabanda ya
kuku, mbuzi, nguruwe, njiwa wala ng’ombe.
Kwa mazingira hayo
wananchi wa Kigamboni itabidi wawapishe wageni na wao wasonge mbele huko
Chekeni Mwasonga na Tundwi Songani wanakoweza kulima, kufuga na
kuendesha mikokoteni.
Tuache kudanganyana hapa eti kuna mtu ana
uchungu na watu wa Kigamboni. La msingi tu watu walipwe vizuri, si kama
walivyodhulumiwa wenzetu wa upande wa Kurasini. Serikali iliwalipa
shilingi milioni 20 kwa eka yenye wakazi 10 hadi 20. Serikali imeuza
maeneo yale baada ya miezi isiyozidi sita kwa wawekezaji kwa shilingi
milioni nyingi.
Na wala watu wasitukumbushe yaliyojiri mwaka
2005 kuhusu daraja hilohilo. Juhudi za kuanza ujenzi Oktoba 2005
zilikwamishwa na kwa sababu ambazo hazijawahi kuwekwa wazi. NSSF nadhani
wanakumbuka kilichotokea wakati ule licha ya maandalizi yote kuwa
yalikuwa yamekamilika.
Tulitangaziwa ya kuwa imepatikana
kampuni ya Kichina iliyojenga huko kwao daraja la urefu wa kilomita 30.
Watu wakajinadi kwamba Wachina hao wangeweza kutumia muda mfupi sana
kujenga daraja la Kigamboni. Lakini mradi uliyeyuka kama theluji kwenye
kiangazi.
Walawale waliokwamisha ujenzi wa daraja huko nyuma
leo wanatamba hadharani na kudai Dk. Ramadhani Dau apewe nishani ya
utendaji bora. Historia ni hakimu makini sana, watu wasifikiri wanaweza
kujifanyia watakavyo halafu historia ikawasamehe.
La msingi ni
kwamba, kama vile tunavyojinadi kuwa tunafuata utawala wa sheria basi
zoezi lile la mji mpya Kigamboni liende kwa kufuata sheria zilizopo.
Hiyo ni pamoja na wananchi kushirikishwa kama sheria zinavyotaka. Lakini
kwa usiri na ubabe huu unaotawala zoezi zima la mradi wa mji mpya
Kigamboni, lazima hoja za kwamba eneo ameuziwa Bush zitaendelea
kujitokeza.
Kama si kweli Bush kauziwa eneo la Kigamboni, usiri
na ubabe, na hoja ya nguvu badala ya nguvu ya hoja vinatoka wapi?
Ukweli (reality) unaiishi independent of the subject, si hoja nani
anasema; rangi yake, cheo chake, umri wake nk. Hivyo basi, ukweli kuhusu
mazingira yanayozunguka mradi wa Kigamboni kama ilivyokuwa kwa EPA,
Richmond, Dowans, Simbion, Tangold, Deep Green na mingine mingi utakuja
kujipambanua na hatimaye kujulikana tu.
Ole wao wanaojifanya
manabii wa injili hii ya Blue Diamond. Watu wasije kulia na kusaga meno
ufunuo utakapofunika sayari hii na hila zao kuwekwa hadharani.
No comments:
Post a Comment