Rais Kikwete anapofikiri kama Kabwe Zitto
Evarist ChahaliUskochiToleo la 261 RAIA MWEMA
3 Oct 2012
NIMEKUWA nikiulizwa swali hili takriban kila wiki baada ya makala zangu
kuchapishwa katika jarida hili maridhawa: Hivi kuna wakati unaishiwa na
cha kuandika? Na siku zote jibu langu linakuwa lile lile; Tanzania yetu
haiishiwi mambo yanayopaswa kujadiliwa-iwe gazetini, mtandaoni,
kijiweni au popote pale. Kuweka rekodi sawia, kila ninapoingia mtandaoni
huwa ninakumbana na wastani wa angalau habari tano zinazoweza
kutengeneza mada za makala zangu.
Wiki hii nitazungumzia
matukio mawili makubwa yanayoihusu CCM na CHADEMA. Kwa namna moja au
nyingine, matukio yote mawili yanahusiana, na nitajitahidi kuonyesha
uhusiano wao mwishoni mwa makala haya.
Tukio la kwanza ni kauli
ya Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kwamba CCM
haitokufa, na pengine wanaodhani hivyo wanaweza kufa wao kabla ya chama
hicho tawala kufa.
Kwa baadhi yetu tunaosoma siasa kama eneo la
taaluma, tunatambua ukweli mmoja, kwamba chama cha siasa kinazaliwa,
kinakua, na kama ilivyo kwa binadamu, kinaweza kufa. Na tofauti na
binadamu ambao hatuna udhibiti mkubwa wa kurefusha au kufupisha maisha
yetu (kuna watenda dhambi na wanaotumia kila aina ya ‘sumu’-pombe, dawa
za kulevya na kadhalika ama kumkera Muumba au kuharibu afya zao-lakini
si tu wapo hai bali pia wana afya za kuridhisha, huku wengine mambo yao
yakizidi kuwanyookea, huku upande mwingine kukiwa na wacha Mungu,
wanaojali afya zao lakini wanataabika muda huu); Vyama vya siasa
vinaweza kurefusha maisha yao kwa kuitumikia jamii kulingana na
matarajio ya jamii husika au ikaipuuza jamii hiyo na kujichimbia kaburi.
Pamoja na heshima yangu kubwa kwa Rais Kikwete, ninaomba kutofautiana
naye katika kauli hiyo kuwa CCM haitokufa. Si tu kuwa vyama vya siasa
hufa, bali pia ninaamini kuwa kila Mtanzania anayefuatilia kwa karibu
historia na mwenendo wa chama hicho anaweza kabisa kubashiri kuwa ama
mwanzo wa mwisho wake unakaribia au kinaharakisha kifo chake.
Simlaumu Rais Kikwete kwa kauli hiyo kwa sababu kama Mwenyekiti wa Taifa
wa Chama anachoongoza ana jukumu kubwa la kuwahakikishia viongozi na
wanachama wenzake kuwa ‘mambo si mabaya’ kama inavyoelezwa na wapinzani
wao.
Binafsi, nasema kinachoweza kuiua CCM kabla ya wakati
wake, ni pamoja na mtizamo huo wa Rais Kikwete wa kwamba ‘chama hicho
kipo imara na kinaendelea kupendwa na Watanzania wengi-uthibitisho (kwa
mujibu wao) ni idadi ya wana-CCM waliojitokeza kugombea nafasi
mbalimbali kwenye chaguzi zinazoendelea ndani ya chama hicho.
Ni kweli kwamba idadi ya waliojitokeza kugombea inaweza kujenga picha
kuwa CCM bado kinapendwa na wengi. Lakini haihitaji ufahamu mkubwa wa
siasa zetu kumaizi kuwa baadhi ya wanaokimbilia uongozi ndani ya chama
hicho wana ajenda zao binafsi. Ikumbukwe kuwa huko nyuma chama hiki
kilishaonyesha dhamira ya kutenganisha biashara na siasa, hatua
iliyotafsiriwa na wengi kuwa ni kutambua kuwa kuna kundi la
wafanyabiashara wanaokimbilia kwenye siasa si kwa minajili ya kuutumikia
umma, bali kusaka ‘kinga’ ya kuwalinda katika biashara zao.
Binafsi, nilikuwa miongoni mwa wapinzani wakubwa wa wazo hilo, si tu kwa
sababu siafikiani na aina yoyote ya ubaguzi, bali pia sikuona kuwa
tatizo ni wafanyabiashara kujihusisha na siasa bali wafanyabiashara
‘wachafu’ kuruhusiwa kujihusisha na siasa. Kwa kuharamisha biashara
kwenye siasa kungeweza kuwa na hatari ya kuwakwaza wazalendo wazuri tu
ambao walichagua kujihusisha na biashara kabla ya kuingia kwenye siasa.
Na ingekuwa ubaguzi wa wazi kuwazuia wafanyabiashara kujihusisha na
siasa, lakini kuwaruhusu askari wastaafu, wasomi na wanajamii wengineo
kufanya hivyo. Sawa, wanasema samaki mmoja akioza basi wote wameoza,
lakini usemi huu hauzingatii ukweli kwamba binadamu hutofautiana.
Kwa mfano, kwa vile Mndamba wa kwanza kumfahamu ni mie ambaye pengine
ninakukera na kwa mtizamo wangu haimaanishi kuwa kila Mndamba
utakayekutana nae maishani atakukera. Waingereza wana msemo kuwa “people
vary because we differ” yaani watu huwa na tofauti kwa sababu
wanatofautiana, na kwa mantiki hiyo hiyo, mfanyabiashara anayeingia
kwenye siasa kwa minajili ya kujitengenezea kinga katika ufisadi wake
kwa taifa, haimaanishi kuwa kila mfanyabiashara anayeingia kwenye siasa
ana malengo hayo.
Ninaamini kilichopelekea CCM kudhamiria
kumtenganisha biashara na siasa ni historia na uzoefu iliopata kutoka
kwa baadhi ya wafanyabiashara walioingia kwenye siasa. Na wazo lilikuwa
zuri, kwamba mfanyabiashara atakayeamua kuingia kwenye siasa achague
moja: biashara au siasa.
Tukirejea kwenye tamko la Kikwete kuwa
CCM haitokufa, yayumkinika kuamini kuwa kauli hiyo ni ya kujipa
matumaini tu na kukwepa ukweli kwamba kwa kiasi kikubwa chama hicho
kinaonekana machoni mwa baadhi ya Watanzania kuwa ni chanzo cha matatizo
mengi yanayoikabili nchi yetu. Kwa kifupi, kitakachoiua CCM si kauli za
hao wanaoikitabiria kifo bali matendo ya chama hicho ambayo kimsingi
ndio ‘pumzi’ inayokifanya kiwe hai.
Tukio jingine ambalo kwa
namna moja au nyingine linahusiana na uhai wa chama cha siasa (kwa maana
ya kuwa hakitokufa au la) ni tamko la Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto
Kabwe (CHADEMA), ya kwamba hatogombea ubunge katika uchaguzi mkuu ujao
wa 2015, bali atagombea urais.
Kwanini ninalinganisha tamko la
Zitto na kauli ya Mwenyekiti wa CCM, Kikwete? Jibu fupi ni kwamba
matamko yote mawili yanaelekea kupuuza hali halisi ya mwenendo wa siasa
za huko nyumbani.
Wakati Mwenyekiti Kikwete anajigamba kuwa CCM
haitokufa japo kuna mamia kwa maelfu ya wana-CCM wanaokihama chama
hicho kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wake, huku pia baadhi ya
viongozi wa chama hicho kama kina Samuel Sitta wakionyesha hadharani
‘maovu’ ya chama hicho, Zitto hataki kujihangaisha kutambua wengi wa
Watanzania wanamtaka mwanasiasa gani kutoka chama chake ili kubeba
dhamana ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Kabla
sijaendelea kuijadili kauli ya Zitto, ningependa kuweka bayana masuala
matatu ya msingi. Kwanza, Zitto ana kila haki si tu ya kutaka kuwa Rais
wa Tanzania, bali pia kutangaza kuwa ana nia hiyo. Ni haki yake ya
kidemokrasia, hasa ikizingatiwa kuwa anatoka katika chama cha Demokrasia
na Maendeleo.
Pili, ni suala la kukubalika kwa wapiga kura
watarajiwa (potential voters). Kila mara ninapomsikia Zitto akielezea
dhamira yake ya kutaka kuwa Rais, huwa ninajiuliza swali moja la msingi;
ni lini amefanya ‘utafiti’ wa kutambua Watanzania wanamhitaji awe rais
wao?
Wenzetu huku Magharibi, kabla mwanasiasa hajakurupuka
kutangaza kuwa anataka kuwa rais huwa inamlazimu kujihangaisha ‘kusoma
upepo,’ yaani kufahamu iwapo wapigakura wanamhitaji.
Sawa,
Tanzania si nchi ya Magharibi, na pengine hakuna umuhimu wa kusaka
mtizamo wa wapigakura. Lakini kwa mwanasiasa anayejali maslahi ya chama
chake na wananchi kwa ujumla, yayumkinika kuamini kuwa atajihangaisha
kufahamu iwapo dhamira yake ya kugombea ni kwa maslahi ya chama chake na
umma kwa ujumla au ni kwa ajili ya kutimiza ndoto zake binafsi tu.
Suala la tatu, na ambalo kwangu si tu ni la msingi zaidi bali pia
linanishawishi kuamini kuwa dhamira ya Zitto kugombea urais ni sawa na
kubariki ushindi wa CCM hapo 2015, ni uadilifu wa mwanasiasa huyo.
Ninamfahamu Zitto vizuri, na si kupitia social media. Ni mmoja wa
wanasiasa wachache wenye kipaji cha hali ya juu katika ujenzi wa hoja.
Lakini, kama mwanadamu mwingine, mwanasiasa huyo ana mapungufu fulani.
Kwa wanaomfahamu kupitia social media (hususan Twitter) wanaweza
kuafikiana nami kuwa si mwepesi sana wa kuafikiana na watu wenye mtizamo
tofauti na wake.
Ni rahisi kumhukumu kuwa ana jazba (japo
sitaki kuamini hivyo) pindi mtu anapotofautiana naye katika anachoamini
yeye kuwa ni sahihi. Nafasi haitoshi kutoa mifano halisi, lakini
waliotofautiana nae kimtizamo ndani ya Twitter wanaweza kuwa mashahidi
wazuri.
Tatizo la msingi kuhusu Zitto ni ‘tuhuma’ zilizowahi
kuandikwa na jarida moja la kila wiki kwamba katika kipindi cha kuelekea
uchaguzi mkuu uliopita, jarida hilo lilinasa mawasiliano kati ya
mwanasiasa huyo na mmoja wa viongozi wa juu wa Idara ya Usalama wa
Taifa.
Katika mazingira ya kawaida, mwanasiasa wa chama cha
upinzani kuwa na mawasiliano na mtumishi wa taasisi hiyo nyeti (ambayo
ilishutumiwa na CHADEMA-ambayo Zitto ni mbunge wake-kuwa ilikihujumu
chama hicho kwenye uchaguzi huo) inazua maswali kadhaa.
Ndio,
watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa ni Watanzania wenzetu kama ilivyo
kwa wanasiasa wa vyama vya upinzani. Lakini mawasiliano kati ya
mwanasiasa wa chama cha upinzani kama Zitto na kiongozi wa idara hiyo,
yanaweza kuibua maswali mengi. Kibaya zaidi, Zitto hajawahi kutoa
‘maelezo ya kueleweka’ kuhusu mawasiliano hayo.
Kimsingi, Zitto
anatambua bayana hisia zilizojengeka baada ya habari hiyo kuchapishwa.
Kuna waliotafsiri kuwa mawasiliano hayo yalilenga kukihujumu chama
hicho, na kwa kuzingatia mantiki ya kawaida tu hatuwezi kuwalaumu kwa
hisia hizo.
Lakini pengine kubwa zaidi ni kwanini bado kuna
idadi kubwa tu ya wafuasi wa CHADEMA wanaotafsiri uamuzi wa Zitto kutaka
urais kama ‘tamaa ya madaraka.’ Hivi akiweka kando imani yake kuwa ana
uwezo na uadilifu wa kuongoza taifa la Tanzania, Zitto ameshawahi
kufikiria kuwashawishi sceptics hawa hata kama hoja zao hazina mashiko?
Kubwa zaidi ni ukweli kwamba matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita
yanaonyesha bayana jinsi mgombea urais kupitia CHADEMA, Dk Willibrod
Slaa, alivyokubalika kwa idadi ya kuridhisha tu wapiga kura. Kama
dhamira ya Zitto ni kuona CHADEMA inaingia Ikulu, kwanini asiwekeze
jitihada kumsapoti Dk Slaa katika uchaguzi ujao na kusubiri ‘zamu yake’
hasa kwa vile umri bado unamruhusu hata kwa miaka mingine 15 ijayo?
Kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano, mgombea urais
sharti awe na miaka 40. Mwaka 2015 Zitto atakuwa na umri pungufu na huo.
Hivi kung’ang’ania kuwa anataka kugombea ilhali akijua Katiba
haimruhusu si ni dalili ya tamaa ya madaraka?
Nimalizie makala
haya kwa kulinganisha matukio mawili haya niliyozungumzia. Kama ambavyo
Rais Kikwete hataki kujiuliza kwanini baadhi ya watu wanaitabiria kifo
CCM, Zitto hataki kujiuliza kwanini baadhi ya watu wanatafsiri dhamira
yake ya kutaka urais mwaka 2015 kama mikakati wa kuirejesha CCM
madarakani na kuinyima CHADEMA nafasi hiyo.
Suluhisho katika
masuala hayo mawili, linaweza kupatikana katika busara hii ya Waingereza
isemayo “never ever put emotions in front of common sense” (kwa tafsiri
isiyo rasmi, kamwe usitangulize hisia mbele ya tabasuri/ busara).
No comments:
Post a Comment