Zitto anataka kusaliti CHADEMA
MWANAHALISI NOV 24,2010
MKUTANO wa kwanza wa Bunge la kumi uliomalizika Alhamisi iliyopita, mjini Dodoma, umeandika historia.
Ni kwa wabunge wa chama kikuu cha upinzani nchini – Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kususia hotuba ya rais Jakaya Kikwete
na kutoka nje ya ukumbi wa bunge.
Hilo ni tukio la kwanza kumkuta rais wa Jamhuri tangu taifa hili lipate uhuru, miaka 50 iliyopita.
Wengi wamezungumzia tukio hilo, lakini wengi wao, wamejikita katika kulaumu CHADEMA.
Bali, tukio lile lina sura nyingi za kujadiliwa. Kwa mfano, kuna rais
anayesusiwa; aliyejibu ususaji kwa njia ya vijembe na kejeli; na kuna
wabunge waliozomea badala ya kusikitika.
Kuna waziri mkuu
anayelaumu na kulaani badala ya kuchukua hatua kabla ya tukio lenyewe
kutokea; kuna serikali iliyoshindwa kuongea na viongozi wa CHADEMA ili
kumuepusha mkuu wa nchi na aibu iliyompata.
Yupo spika
“mwanafunzi” ambaye ameshindwa kufanya jitihada zozote za wazi kuepusha
aibu iliyotokea na ambayo imemfunika yeye na historia yake aliyoiweka
siku chache zilizopita.
Kuna CHADEMA na uamuzi wa kutumia njia
ya kususia badala ya kutumia nyingine kama kweli zilikuwepo. Vipo vyama
vingine vya upinzani ambavyo badala ya kusikitika, viliinuka kuchukua
viti vilivyoachwa wazi na CHADEMA.
Kwa ujumla, tukio lile
lilikuwa na sura nyingi, lakini ushabiki wa baadhi ya waliojitosa
kujadili, umewanyima wananchi wengi fursa ya kuchambua na kujadili sura
hizo kwa faida ya vizazi vijavyo.
Makala hii, nayo haitajadili
hayo. Badala yake, itajikita katika mjadala ulioibuliwa na mbunge wa
Kigoma Kaskazini (CHADEMA), naibu katibu mkuu wa chama hicho na naibu
kiongozi wa upinzani bungeni, Zitto Kabwe.
Yeye na baadhi ya wabunge wenzake wachache waliamua kutoingia bungeni kinyume na maelekezo ya chama chao.
Katika utetezi na ufafanuzi alioutoa kupitia televisheni ya taifa
(TBC1), Zitto anadai pamoja na mengi, kuwa yeye na wenzake waliamua
kutoingia ukumbini kuepuka kumwaibisha mkuu wa nchi ambaye ni Amiri
Jeshi Mkuu.
Kwamba, aliamua kufuata dhamiri na shinikizo la
wapiga kura wake ili kuonyesha heshima kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye
amefanya maendeleo makubwa mkoani Kigoma kuliko rais yeyote tangu uhuru.
Kwa Zitto, maendeleo mkoani Kigoma ni fadhila kutoka kwa rais na
anajisikia deni mbele yake. Alihitimisha kwa kusema, “Rais ni alama ya
umoja wa nchi na ni lazima aheshimiwe.”
Kabla ya utetezi wake,
kulikuwa na taarifa kwamba Zitto alikuwa “anatumika” kushawishi wabunge
wagawanyike katika suala la msimamo mmoja wa chama chao. Ilimlazimu
kutumia hata udini ili kukamilisha adhima yake.
Kwa kuwa suala
la udini alilizungumzia pia katika mahojiano yake na TBCI, nashawishika
kuamini kuwa Zitto anayo ajenda ya udini katika kutimiza malengo yake ya
kuigawa CHADEMA.
Iwe anayo yeye kama yeye, au anatumwa na
wanaomtuma, kuna kila sababu ya kuamini kuwa Zitto ametekwa na fikra
hizi mbaya za udini anaodai anaupinga.
Fikra hizi ni matusi kwa
wananchi waliomchagua kutokana na kuamini kuwa ana uwezo wa kuongoza.
Kumbe moyoni mwake anaamini kuwa alichaguliwa kwa misingi ya udini!
Kwa mwanasiasa kijana, msomi na aliyewahi kujijengea heshima siku za
nyuma, hatua hii inawasaliti maelfu ya vijana waliokuwa na matumaini
makubwa kwake, kwani wanaona kauli na vitendo vyake vinachonga jeneza
lake na fikra zake.
Naendelea kumwamini hayati Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyesema kuwa wanasiasa waliofilisika
au wanaoelekea kufilisika, hujificha ndani ya kwapa la udini na ukabila.
Kwa hili, Zitto amefilisika mapema wakati biashara ya siasa ndiyo inaanza.
Siku mbili kabla ya tukio la bungeni, Zitto alikuwa na mazungumzo ya
muda mrefu na alikuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na waziri mkuu
aliyejiuzulu, Edward Lowassa na baadaye akafanya mazungumzo na Rais
Kikwete kwa njia ya simu.
Habari hizi alizisema Zitto mwenyewe ili kuwashawishi wabunge wakubaliane naye katika “mpango” wake wa kukigawa chama chake.
Baadaye alikutana na “maofisa maalum” wa serikali aliodai kuwa walikuwa
wanampa habari maalum za kusaidia kumaliza aibu ambayo ingetokea kwa
kususia hotuba ya rais. Wanafahamika hata kwa majina.
Kwa ujumla, Zitto alionekana kumhurumia Kikwete kuliko hata Chama Cha Mapinduzi (CCM) chenyewe kinavyomhurumia mwenyekiti wake.
Kwa mtu yeyote anayejali na kupenda kuimarisha siasa mbadala katika
nchi, atasikitika kusikia na kuona haya yakifanywa na Zitto.
Hata kama upinzani si uadui, lakini upinzani unaojipendekeza kwa CCM
kuliko hata wana-CCM wenyewe ni wa hatari; na wanachama wenyewe wa CCM
hawautaki.
Wana-CCM makini hawapendi tabia ya Zitto
kujipendekeza kwa viongozi wa juu na wakati mwingine kuwachonganisha kwa
kuvujisha habari azipatazo kutoka kwa mmoja kwenda kwa mwingine.
Tayari hatua ya Zitto ya kuchukua maneno ya huyu na kumpa yule, imechochea mgogoro wa chinichini ndani ya chama cha Kikwete.
Mgogoro huu unapata nguvu kutokana na utamaduni mpya wa mtendaji mkuu
wa CCM, Yusuph Makamba kuthamini wapinzani mamluki wanaorejea CCM baada
ya kuwa wameshakibomoa chama hicho kwa kukishushia lundo la shutuma.
Orodha ya wanaopewa kipaumbele na Makamba kuliko wanachama wengi
wanaojitolea kujenga chama chao, inahusisha Steven Wasira, Tambwe Hizza,
Mbarouk Msabaha, Dk. Amani Kaborou, Sahibu Akwilombe, Daniel
Nsanzugwanko, Justine Sarakana na Thomas Ngawaiya.
Ndani ya chama cha Makamba na Kikwete, hawa ni wanachama wanaotoka daraja tofauti.
Naye Zitto anaelekea kupenda kujiunga na orodha hiyo kwa gharama mbili
kubwa. Kwanza, kwa kuigawa CHADEMA (yenyewe kwa yenyewe) na pia CHADEMA
na wapinzani wengine.
Pili, anaelekea kuanzisha migogoro ya
ndani ya CCM kwa sababu anadai anayoyafanya ndani ya CCM anakuwa na
ridhaa ya kiongozi mkuu wa chama – Makamba.
Wenye akili wanajua
kuwa baadhi ya madai yake si ya kweli. Lakini hata yale machache yaliyo
ya kweli, hayana dhamana ya chama hicho, bali utashi binafsi wa mmoja
wa viongozi ndani ya chama hicho.
Katika suala la uadilifu kwa
chama, CCM ikiwa taasisi, haina mwanachama aliye juu ya sheria hata kama
wapo watu wengi nje ya chama hiki ambao wanaweza kupinga dai hili.
Kwa mfano, sidhani kama Zitto ana thamani kubwa ndani ya CCM kuliko
Lowassa ambaye pamoja na mengi makubwa aliyokifanyia chama chake, bado
wamegoma kumsafisha kutoka katika tuhuma zilizosababisha ateme kiti
chake cha uwaziri mkuu.
Wala sidhani kama Zitto ni bora kuliko
Samweli Sitta ambaye licha ya kuweka rekodi nzuri ya kusimamia bunge, ni
CCM iliyosema Sitta hafai tena kuwa spika.
Ni Sitta na Lowassa
waliofanikisha “kampeni za kisayansi” zilizomwingiza Kikwete madarakani
mwaka 2005, lakini ni Kikwete huyohuyo aliyesema Sitta hafai na
anaelezwa kila siku hadi asadiki kuwa Lowassa hasafishiki.
Mifano hii inatosha kumfundisha Zitto kuwa yuko hatarini pale
anapojifanya na kudai kumheshimu mwenyekiti wa CCM kuliko anavyomheshimu
mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.
Usaliti ambao Zitto anaufanyia CHADEMA ni huohuo atakaoifanyia CCM endapo atajiunga na chama hicho.
Inavyoelekea si siku nyingi kutoka sasa Zitto atajisajili katika CCM ambayo anaitumikia sasa kwa mlango wa nyuma.
Nitakuwa wa mwisho kumkaribisha Zitto ndani ya CCM. Chama cha CCM kiko
tayari kumtosa yeyote hata kama kwa kufanya hivyo kinapata hasara.
Zitto hajachelewa kuachana na utoto huu kwa kuheshimu chama chake
ambacho, siyo tu kinaheshimiwa bali hata kuogopwa na wengi wakiwamo
baadhi ya viongizi wakuu wa CCM.
Vinginevyo, Zitto awe tayari kuangamia.
No comments:
Post a Comment