Polisi yawashikilia viongozi wa Uamsho
JESHI la Polisi visiwani Zanzibar linawashikilia viongozi watano wa
Taasisi za Kiislamu Zanzibar, akiwamo kiongozi wake, Sheikh Farid Hadi
Ahmed.
Viongozi hao wako mikononi mwa polisi tangu juzi wakihojiwa
kuhusiana na tukio la kutoweka kwa kiongozi huyo ambaye ilidaiwa kuwa
alikamatwa na ‘kufichwa’ na polisi kwa siku nne.
Kamishna wa
Polisi wa Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema jana kwamba wamewakamata na
kuwahoji na watawafikisha mahakamani leo iwapo wataridhika kama wana
mashtaka ya kujibu.
Mbali na Sheikh Farid, vigogo wengine ambao
wanashikiliwa na polisi ni Mkuu wa Uamsho, Sheikh Mselem Ali Mselem,
Naibu wake, Azzan Khalid Hamdan, Mussa Juma na Hassan Bakari.
Uamsho wasisitiza amani
Wakati
jeshi hilo likiendelea kuwahoji viongozi hao, taasisi hiyo imetoa
waraka wa kuwataka Waislamu wadumishe amani hasa katika kipindi hiki
ambacho viongozi hao wanashikiliwa na jeshi hilo.
Waraka huo
uliotolewa jana na kusambazwa katika misikiti mbalimbali kisiwani hapa,
umewataka Waislamu wawe watulivu na kuhudhuria kwa wingi mahakamani leo
wakiwa na vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.
Waraka huo unasema:
“Kama hali ilivyo na mnavyosikia mnaombwa muwe watulivu na mfanye subira
na leo (jana) hapo Msikiti wa Mbuyuni hapatakuwa na muhadhara si
Adhuhuri wala Alasiri. Mnachoombwa na viongozi wenu muwe wavumilivu na
watulivu hadi kesho (leo), mfike mahakamani bila ya fujo na muchukue
kopi (nakala) za vitambulisho vyenu vya Mzanzibari.”
“Jingine ni
kuwa msikae vikundi na mkawapa askari sababu, tunasisitiza amani na
utulivu na Waislamu ni wenye kutii amri za viongozi wao. Tunasisitiza
amani na utulivu, pia subira na dua kwa wingi. Ukipata taarifa hii
mjulishe na mwenzio toa nakala na uwape wengine. Wabillah Taufiq.”
Hata
hivyo, waraka huo ambao ulikuwa unasambazwa katika misikiti jana
haukutiwa saini na kiongozi yeyote wala haukutaja umetolewa na nani.
Wakili
wa Uamsho, Salim Tawfik alisema jana kuwa wateja wake watafikishwa
mahakamani leo, lakini akalaumu kwamba polisi wamewahoji bila ya yeye
kuwapo.
“Mimi nilikwenda polisi nikakuta Mselem anahojiwa nikataka
kuingia wakanizuia, wakasema wataniita lakini hawakufanya hivyo,”
alisema.
Hali ya Zanzibar kwa sasa imetulia ingawa polisi na
askari wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), wameimarisha
ulinzi katika maeneo mbalimbali wakiwa wanazunguka kuhakikisha hali
inaendelea kuwa shwari.
Kwa siku tatu mfululizo, Mji wa Zanzibar
ulikumbwa na ghasia kubwa kwa askari kupambana na wananchi ambaowalikuwa
wakiandamana wakitaka Sheikh Farid aachiwe huru wakidai amekamatwa kwa
kificho na polisi jambo ambalo jeshi hilo ililikanusha.
Juzi, kiongozi huyo alijitokeza hadharani na kudai kuwa alichukuliwa na polisi na kumrudisha mahali walipomchukua.
No comments:
Post a Comment